Farida Mangube, Morogoro
Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Bi Pili Mnyema, ameitka Kampuni ya Ranchi za Taifa NARCO kushirikiana na wafugaji wadogo kwa kuwapatia elimu, mbegu bora za mifugo, na kuwahusisha katika mnyororo wa thamani wa mifugo ili kukuza mazao ya mifugo na kuchochea uchumi wa ndani na kutoa ajira kwa vijana.
Bi Mnyema ameyasema hayo alipotembelea banda la NARCO katika Maonesho ya 88 ya Kanda ya Mashariki yanayofanyika mkoani Morogoro, huku akiipongeza taasisi hiyo ya serikali ambayo imekuwa chachu ya mageuzi katika sekta ya mifugo na viwanda vya nyama nchini.
Bi Mnyema alijionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na NARCO zikiwemo ufugaji wa kisasa, usindikaji wa nyama, na uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na mifugo. Alieleza kufurahishwa na namna taasisi hiyo inavyotekeleza majukumu yake kwa weledi, ubunifu, na kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.
“Nimeridhishwa sana na kazi yenu. Mnafanya kazi ya kisasa, inayoweka Tanzania mbele katika ubora wa uzalishaji wa nyama. Hii ni hazina ya taifa ambayo tunapaswa kuilinda na kuikuza,” alisema Bi Mnyema.
Kwa upande wake Meneja wa NARCO Mkata Oscar Mengele amesema kuwa kampuni hiyo inamiliki jumla ya ranchi 15 zilizotapakaa katika mikoa mbalimbali ya nchini, ambazo zote zinajihusisha na uzalishaji wa mifugo bora kwa ajili ya nyama na mazao mengine.
Amesema ranchi hizo ni pamoja na Kongwa Ranch iliyopo mkoani Dodoma, ambayo ni maarufu kwa nyama yake yenye ubora wa kipekee, Ruvu Ranch mkoani Pwani, Misenyi na Missenyi (Murongo) Ranch zilizopo Kagera, Mabwegere Ranch ya Morogoro, Kalambo Ranch ya Rukwa, Kikulula Ranch ya Geita, Usangu, Mpongwe, na Mbalali Ranches zote za mkoa wa Mbeya.
Nyingine ni pamoja na Mkata, Ngerengere zilizoko Tanga na Morogoro Kitulo Ranch Njombe, Kagoma Ranch ya Kigoma, na Manyara Ranch ya mkoa wa Manyara huku ranchi zote zikiwa zimeboreshwa ili kufanikisha uzalishaji wa kisasa unaolenga soko la ndani na nje ya nchi.
Aidha ameongeza kuwa nyama ya Kongwa, inayotoka katika Kongwa Ranch mkoani Dodoma ni moja ya biadhaa zao zilizojizolea umaarufu mkubwa kutokana na ladha yake ya asili, muonekano wake wa kuvutia, na virutubisho vya asili vilivyomo ndani yake.
“Kongwa Ranch imekuwa ikitajwa mara kwa mara kama mfano wa mafanikio ya NARCO, na nyama yake sasa inahitajika katika hoteli, taasisi, na masoko mbalimbali ya ndani na hata ya kimataifa”. AmesemaMengele
“Kongwa imekuwa kitovu cha ubora. Tumepokea oda kutoka sehemu mbalimbali nchini na tunapokea maombi kutoka nje pia. Hii inaonesha kuwa Tanzania inaweza kuzalisha nyama bora kwa viwango vya kimataifa bila kuagiza kutoka nje,” aliongeza.