Mtafiti idara ya Korosho kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo Tanzania Naliendelea Mkoani Mtwara Abdala Makale kulia,akitoa elimu juu ya kilimo cha Korosho kwa Maafisa tarafa,Watendaji kata,Wenyeviti wa Vijiji na Wanafunzi wa shule za Msingi kutoka Halmashauri ya Wilaya Mbinga waliotembelea banda la TARI kwenye maonyesho ya Wakulima Nane nae yanayofanyika katika kijiji cha Amanimakolo Wilayani humo.
Na Mwandishi Wetu,Mbinga
TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania(TARI)Kituo cha Naliendele Mkoani Mtwara,kimeendelea kutoa elimu kwa wakulima wa Mkoa wa Ruvuma kuhusu kanuni za uzalishaji na umuhimu wa kutumia mbegu bora zilizofanyiwa utafiti ili waweze kulima kwa tija.
Akizungumza na wakulima katka kijiji cha Amanimakolo Wilayani Mbinga,Mtafiti wa Kilimo wa TARI Kituo cha Naliendele Mkoani Mtwara Stella Massawe alisema,lengo la Taasisi hiyo kushiriki maonyesha hayo kwa ajili ya kutoa elimu na kuwajengea uelewa wakulima umuhimu wa kutumia mbegu bora ili kuongeza uzalishaji.
Alisema,TARI inajihusisha na kilimo kwa kufanya utafiti wa mbegu, kuzalisha mbegu na kuongeza thamani mazao mbalimbali yanayozalishwa na wakulima hapa nchini.
Kwa mujibu wa Massawe,Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa inayozalisha chakula kwa wingi hapa nchini, lakini tija ni ndogo kutokana na baadhi ya wakulima kutumia mbegu za kienyeji ambazo hazijafanyiwa utafiti.
“tunamshauri mkulima kwanza afahamu zao analotaka kulima,anapata mbegu wapi na atambue njia sahihi ya kilimo cha kisasa ili aweze kuzalisha mazao mengi na bora kwa ajili ya kujiongezea kipato”alisema Massawe.
Aidha alisema,TARI ina vituo 17 hapa nchini vilivyoanzishwa kwa ajili ya kutoa ushauri na utafiti wa mbegu za kilimo cha korosho ambacho kama kitasimamiwa vizuri zao hilo litachangia kukua kwa uchumi wa mkulima mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Alisema, vituo hivyo vimeanzisha ili kuhakikisha elimu ya zao la korosho inafikishwa karibu kwa ajili ya kuwaondolea wakulima usumbufu kwenda mbali kwa ajili ya kupata elimu sahihi ya zao hilo la kimkakati hapa nchini.
Alisema,katika Mkoa wa Ruvuma kuna vituo vitano vya uendelezaji wa zao la korosho vilivyopo katika kijiji cha Nandembo na Chikomo Wilaya ya Tunduru,Paradiso Wilaya ya Mbinga na Lusewa Wilaya ya Namtumbo.
Alisema,mpaka sasa TARI imegundua aina 62 za mbegu bora ya korosho zilizoanza kupandwa na wakulima katika mikoa mbalimbali hapa nchini pamoja na utafiti wa mbegu za karanga na ufuta.
Amewataka wakulima,kufika kwenye banda la Tari ili kukutana na wataalam waliobobea katika tafiti za kilimo ikiwemo kilimo cha zao la korosho.
Naye Mtaalam wa kilimo wa TARI Juma Mfaume alisema,katika maenesho ya mwaka huu wamekuja na mbegu mbalimbali za nafaka ikiwemo mbegu bora ya mtama,mbegu ya ulezi na njungu mawe.
Alisema,lengo la kuleta mbegu hizo ni kwa sababu wakulima wa Mikoa ya Nyanda za juu kusini hususani Mkoa wa Ruvuma wanajihusisha na kilimo cha nafaka na mikunde.
Kwa upande wake afisa kilimo kutoka Halmashauri ya Mbinga Onesifol Mlimba alisema,maonyesho hayo ni muhimu kwa wakulima kwani watapata mbinu za kilimo bora na cha kisasa kuhusiana na zao la muhogo na mazao mengine yanayolimwa kwa wingi katika Mkoa wa Ruvuma.
Alisema,kupitia maonyesho hayo wataalam wa kilimo watapata ujuzi na teknolojia mbalimbali ambazo zitatumika kuwafundisha wakulima ili waweze kulima kisasa, kuzalisha mazao mengi ili kuondokana na umaskini kupitia shughuli zao za kilimo.
“kupitia maonyesho ya nane nane ya mwaka 2025 tunategemea kila kiongozi atakayeshiriki na kufika kwenye banda hili la TARI atakuwa chachu kwa wakulima,maana yake elimu tutakayopata itakuwa chachu kwa kuongeza uzalishaji mashambani”alisema.
Baadhi ya Wakulima wa Kijiji cha Amanimakolo Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma, wakiangalia mbegu za mazao mbalimbali kwenye Banda la Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania(TARI)Kituo cha Naliendeli kwenye maonyesho ya Nanenane ambayo katika Mkoa wa Ruvuma yanafanyika katika Kijiji cha Amanimakolo Wilayani Mbinga.
Wakulima wakiendelea kupata elimu ya mbegu kwenye banda la TARI kwenye maenyesho ya Wakulima Nane nane kijiji cha Amanimakolo Wilaya ya Mbinga.
Mtafiti idara ya Korosho kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo Tanzania Naliendelea Mkoani Mtwara Abdala Makale kulia,akitoa elimu juu ya kilimo cha Korosho kwa Maafisa tarafa,Watendaji kata,Wenyeviti wa Vijiji na Wanafunzi wa shule za Msingi kutoka Halmashauri ya Wilaya Mbinga waliotembelea banda la TARI kwenye maonyesho ya Wakulima Nane nae yanayofanyika katika kijiji cha Amanimakolo Wilayani humo.