Katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umegawa majiko na mitungi ya gesi kwa Maofisa na Askari wa Jeshi la Magereza katika mikoa 14 nchini ili kulinda afya zao kwa kuwaondoa kwenye matumizi ya kuni na mkaa.
Akizungumza Agosti 6, 2025 kwenye hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa jumla ya majiko na mitungi 1,611 katika magereza sita ya Mkoa wa Dodoma, iliyofanyika Gereza la Isanga, Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhandisi Sophia Mgonja amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kusambaza nishati safi kwa Watanzania wote.
“Ni matarajio yetu kwamba Maofisa na Askari mtaendelea kutumia nishati hii safi na kuwa mabalozi kwa jamii nyingine. Tusiwaruhusu kurudi nyuma kwa kutumia tena kuni au mkaa. Hii ni hatua ya kulinda maisha, afya na mazingira,” amesema Mhandisi Mgonja.
Ameongeza kuwa matumizi ya kuni yamekuwa yakihusishwa na changamoto nyingi za kiafya, akitolea mfano wa mkoa wa Shinyanga ambapo wanawake walikuwa wakikumbana na madhara ya macho mekundu kutokana na moshi wa kuni waliokuwa wakitumia kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Jeshi Magereza (ACP) George Wambura, amesema kupokea majiko na mitungi hiyo ni uthibitisho kuwa serikali inajali afya na ustawi wa Maofisa na Askari wake.
“Niwahimize Maofisa na Askari wote, baada ya mitungi hii kuisha gesi, hakikisheni mnaijaza na kuendelea kutumia gesi. Tuchukue hatua madhubuti za kuachana kabisa na matumizi ya kuni na mkaa,” amesema ACP Wambura.
Amebainisha kuwa tangu Desemba mwaka 2024, magereza yote nchini yameanza kutumia nishati safi, na kusisitiza kuwa nishati zisizo safi ni hatari kwa afya, zikiwemo kusababisha magonjwa ya mfumo wa hewa na saratani.
Naye, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Godfrey Chibulunje, amesema Wakala huo uliingia mkataba na Jeshi la Magereza Septemba 2024 wenye thamani ya Shilingi bilioni 35.23 kwa ajili ya kusambaza na kufunga miundombinu ya nishati safi ya kupikia kwenye magereza yote nchini.
“Kwa Mkoa wa Dodoma jumla ya majiko na mitungi 1,611 itatolewa kwa watumishi wa Jeshi la Magereza, ambapo Gereza la Isanga pekee limepokea seti 350 kwa ajili ya Maofisa na Askari wake,” amesema Chibulunje.
Awali, akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Wawekezaji Miradi kutoka REA, Mhandisi Emmanuel Yesaya,
amesema katika mkataba huo REA itasambaza mitungi 15,126 ya kilo 15 na kuwajengea uwezo watumishi wa jeshi hilo kuhusu matumizi ya nishati hiyo.