

Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Agosti 9, 2025, amechukua rasmi fomu za kugombea nafasi hiyo kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Shughuli hiyo imefanyika katika ofisi za makao makuu ya tume, Njedengwa jijini Dodoma, ambapo Mwenyekiti wa INEC, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele, ndiye aliyemkabidhi Dkt. Samia fomu hizo.
Dkt. Samia aliwasili katika ofisi za tume saa 5:20 asubuhi akiwa ameongozana na mgombea mwenza wake, Dkt. Emmanuel Nchimbi, na viongozi wakuu wa chama akiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Zuber Ali Maulid, pamoja na Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda.
Baada ya kukamilisha taratibu za ndani kwa takribani dakika 27, Dkt. Samia alitoka akiwa amebeba begi jeusi lenye maandishi “Fomu za Uteuzi”, ishara ya kukamilika kwa hatua hiyo muhimu katika safari yake ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Nje ya jengo la INEC, mgombea huyo wa CCM alisimama kupiga picha na makundi mbalimbali ya makada na wafuasi wa chama, huku wakiwa na furaha na shangwe kubwa.
Mara baada ya hapo, msafara wa Dkt. Samia na mgombea mwenza wake ulielekea makao makuu ya CCM jijini Dodoma kwa ajili ya kuendelea na ratiba za chama, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea kampeni rasmi.
