

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, amewataka wafanyabiashara wa kati maarufu kama mawinga kuhakikisha wanazingatia sheria za kodi na kujitokeza kulipa kodi kwa wakati.
Akizungumza Agosti 9, 2025 jijini Dar es Salaam, Kamishna Mwenda ametoa wito huo wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Elimu ya Kodi kwa Biashara za Mtandaoni. Uzinduzi huo umehudhuriwa na wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari, wawakilishi kutoka TCRA, BASATA, pamoja na Umoja wa Wafanyabiashara wa Kariakoo.
Kamishna Mwenda amesema kuwa biashara za mtandaoni zimeendelea kukua kwa kasi nchini, jambo linalofanya kuwa muhimu kwa wafanyabiashara wote hususan mawinga na wale wanaouza kwa kutumia mitandao kuelewa umuhimu wa kodi kama sehemu ya kuchangia maendeleo ya taifa.
“Nimesikia wengine wanasema sisi mawinga, mawinga, winga si kamisheni, biashara ya winga ni huduma. Ukifanya biashara la milioni moja na ukaiuza milioni moja na laki moja, hautatozwa laki moja, ila utatusaidia huyo wa milioni moja ni nani ili atozwe kwa milioni hiyo moja”, amesema Mwenda.
Aidha, ameeleza kuwa kampeni hii inalenga kuelimisha na kuwahamasisha wafanyabiashara wote kujiunga rasmi na TRA na kulipa kodi kwa njia sahihi. Alisisitiza umuhimu wa kufuata taratibu za malipo, hasa katika kipindi hiki ambacho biashara za mtandaoni zinaongezeka kwa kasi kubwa.