Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Balozi Simon Sirro,akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA Kanda ya Magharibi, Mhandisi Walter Christopher,mara baada ya kutembelea banda la EWURA wakati wa kilele cha maonesho ya Nanenane, yaliyofanyika katika viwanja vya Ipuli, mkoani Tabora.
Na.Mwandishi Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Balozi Simon Sirro, ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Magharibi kwa kufanikisha utoaji wa elimu na kuwafikia wakulima na wafugaji katika maonesho ya Nanenane, yaliyofanyika katika viwanja vya Ipuli, mkoani Tabora, kuanzia Agosti 1 hadi 8, 2025.
Mhe. Sirro alitoa pongezi hizo Agosti 8, alipotembelea banda la EWURA wakati wa kilele cha maonesho hayo kwa Kanda ya Magharibi, ambayo inajumuisha mikoa ya Tabora na Kigoma.na kueleza kufurahishwa na namna EWURA inavyoshiriki kuboresha upatikanaji wa huduma za nishati na maji nchini.
“EWURA hongereni kwa kuwafikia wakulima na wafugaji,utaratibu huu uendelee, na tuchape kazi,” alisema Balozi Sirro.
Akitoa maelezo kwa mgeni huyo, Meneja wa EWURA Kanda ya Magharibi, Mhandisi Walter Christopher, alisema mamlaka hiyo imekuwa ikitoa elimu kuhusu fursa zilizopo katika sekta za nishati na maji, ili kuwawezesha wananchi, hasa wa vijijini, kuongeza kipato na kushiriki katika miradi ya kimkakati.
“Katika maonesho haya tumewahamasisha wakulima na wafugaji kutumia sehemu ya mapato yao kuwekeza kwenye vituo vya mafuta vijijini, ambako bado kuna uhitaji mkubwa wa huduma hiyo,” alisema Mhandisi Christopher.
Aidha, aliongeza kuwa wamehamasisha wananchi kujisajili katika kanzidata ya watoa huduma, inayoratibiwa na EWURA, ili kupata nafasi ya kushiriki kwenye miradi mikubwa ya mafuta na gesi asilia nchini, ikiwemo mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga.
Hata hivyo Mhandisi Christopher, alisisitiza umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia kwa ajili ya kulinda afya na mazingira, na kuhimiza wananchi kuwekeza katika biashara ya usambazaji wa gesi ya kupikia (LPG), ambapo EWURA hutoa vibali na leseni kwa wajasiriamali wanaotaka kuingia katika sekta hiyo.
Aidha, alieleza pia kwamba, washiriki wa maonesho hayo wamesisitizwa kutumia nishati safi ya kupikia ili kutunza afya na mazingira ikiwemo kuwekeza katika biashara ya usambazaji wa LPG ambapo EWURA hutoa vibali na leseni kuwezesha shughuli hiyo.