
DODOMA – Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kongwa kimetangaza kuanza tena mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu za kuwania nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Kongwa, kufuatia kifo cha aliyekuwa Spika wa Bunge na Mbunge wa jimbo hilo, Job Ndugai, kilichotokea Agosti 6, 2025.
Kwa mujibu wa Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Kongwa, Julius Lepupuma, zoezi hilo litafanyika kwa siku moja pekee, Agosti 12, 2025, kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni, katika ofisi ya CCM Wilaya ya Kongwa, ambapo fomu zitatolewa na Katibu wa Wilaya.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa gharama za fomu zitaendelea kuwa kama zilivyoanishwa kwenye Kanuni za Uongozi katika Vyombo vya Dola toleo la 2025, huku ikisisitiza kuwa waombaji lazima wawe wanachama hai wa CCM, wenye akili timamu, na waliolipia ada ya uanachama.
Aidha, CCM imepiga marufuku maandamano au misafara ya magari, pikipiki, baiskeli, pamoja na matumizi ya ngoma au matarumbeta wakati wa kuchukua fomu. Pia, imekataza kuandaa wapambe kwa sherehe za kusindikiza wagombea.