Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Same–Mwanga (SAMWASA), katika utekelezaji wa operesheni Zuia Upotevu wa Maji (ZUMA), imemkamata mtu mmoja mkazi wa eneo la Stering, kata ya Same, wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, kwa kosa la kuunganisha maji kwa njia ya wizi kinyume cha sheria na kuyatumia kwa muda wa zaidi ya miaka mitatu bila kugundulika.
Akizungumza wakati wa operesheni hiyo, Afisa Bili wa Kanda ya Same, Bi. Sakina Rajab, alisema walimbaini mteja huyo wakati wa msako wa nyumba kwa nyumba wa ZUMA. Uchunguzi umebaini kuwa aliunganisha bomba la siri nyuma ya mita na kuelekeza maji hayo kuingia moja kwa moja kwenye mfumo wa ndani wa nyumba yake, bila mita kusoma matumizi halisi. Kitendo hicho kimesababisha hasara kwa mamlaka na wananchi wengine wanaolipa bili kihalali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa SAMWASA, Mhandisi Rashid Shaban Mwinjuma, amesema mteja huyo anashughulikiwa kwa mujibu wa sheria, akisisitiza kuwa operesheni ya ZUMA ni endelevu na inalenga kudhibiti upotevu wa maji, kuhakikisha huduma inawafikia walengwa, na kulinda miundombinu ya mamlaka.
Aidha, sambamba na kudhibiti vitendo vya wizi wa maji, serikali inaendelea kuwekeza katika ujenzi na upanuzi wa miundombinu ya maji safi, ikiwemo mabomba na vituo vya kusambaza maji karibu na makazi ya wananchi, ili kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo muhimu na kupunguza changamoto za ukosefu wa maji vijijini na mijini.
Wito kwa Wananchi: “Tunawasihi wananchi wote kutumia huduma za maji kwa njia halali, kulipa bili kwa wakati, na kulinda miundombinu ya maji. Wizi wa maji ni kikwazo kwa upatikanaji wa huduma bora na ni kosa kisheria. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuhakikisha maji safi na salama yanapatikana kwa wote,” amesema Mhandisi Mwinjuma.
Uunganishaji maji kwa njia ya wizi au kuchepusha maji kwa udanganyifu ni kosa kisheria kwa mujibu wa Sheria Namba 5 ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2019.