Dar es Salaam: Benki ya CRDB hivi karibuni ilizindua ‘CRDB Al Barakah Sukuk,’ hatifungani inayokusanya fedha ili kuwezesha biashara bila riba nchini na ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.
Hatifungani hiyo inayofuata misingi ya Kiislamu, inakusudia kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 30 pamoja na dola za Marekani milioni 5 huku kukiwa na uwezekano wa kuongeza kiasi hicho mpaka shilingi bilioni 40 na dola milioni 7. Uzinduzi huo unaifanya CRDB Al Barakah Sukuk kuwa hatifungani yenye thamani kubwa zaidi kutolewa na taasisi ya fedha nchini tena ikiruhusu uwekezaji wa sarafu nyingi.

Akizindua hatifungani hiyo mwishoni mwa wiki, Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete ameipongeza Benki ya CRDB kwa jitihada zake za kuhamasisha ujumuishaji kiuchumi wa wananchi wote.
“Hatifungani hii inaleta mapinduzi katika masoko yetu ya mitaji nchini. Inatoa nafasi kwa watu ambao awali walikuwa wameachwa nje ya mfumo rasmi ya fedha kutokana na imani za kidini kwa kuileta fursa hii ya uwekezaji usio na riba unaoendana na misingi ya sharia. Hii ni hatua kubwa katika kuwajumuisha wananchi kiuchumi na maendeleo ya maadili yetu. Ninao uhakika kwamba hatifungani hii itavutia wawekezaji wengi kuliko matarajio mliyonayo kwa sasa,” amesema Rais Kikwete.

CRDB Al Barakah Sukuk ni toleo la tatu la hatifungani za Benki ya CRDB chini ya Mkakati wa Muda wa Kati (Medium Term Strategy) wa 2023–2027 wenye thamani sawa na dola za Marekani milioni 300 uliothibitishwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).
Hatifungani hii imekuja baada ya Hatifungani ya Kijani (Green Bond) na Hatofungani ya Miundombinu ya Samia (Samia Infrastructure Bond) ambazo zote zilivutia wawekezaji wengi kuliko ilivyotarajiwa hali inayothibitisha imani waliyonayo wawekezaji wa ndani na nje ya nchi juu ya ufanisi wa Benki ya CRDB.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Mussa Nsekela amesema: “Hatifungani hii inathibitisha imani yetu kwamba uwezeshaji lazima uwe jumuishi na ukidhi mahitaji ya kila Mtanzania. Kupitia hatifungani hii tunafungua milango kwa watu wengi zaidi kushiriki uwekezaji kupitia masoko yetu ya mitaji bila kuathiri imani zao za kidini. Ni kichocheo cha kuwezesha miradi na biashara zinazozingatia maadili, zilizo endelevu na zinazoinufaisha jamii.”
Nsekela amesema fedha zitakazopatikana kutokana na mauzo ya hatifungani hii zitaelekezwa kuwezesha miradi inazingatia maadili na biashara zisizo na madhara kwa binadamu kulingana na misingi ya sharia ikiwamo inayolenga kutoa huduma za afya, kilimo na ufugaji, elimu na uzalishaji usioathiri mazingira.

“Hatifungani hii inatoa faida ya asilimia 12 kwa mwaka kwa watakaowekeza kwa shilingi na asilimia 6 kwa watakaowekeza kwa dola ya Marekani kwa mwaka. Faida hii italipwa kwa mwekezaji mara nne kwa mwaka yaani kila baada ya miezi mitatu. Mtu binafsi, kampuni au taasisi anaweza kuwekeza kuanzia shilingi 500,000 au dola 1,000 za Marekani. Dirisha la uwekezaji litakuwa wazi kuanzia sasa mpaka Septemba 12,” amesema Nsekela.
British International Investment (BII), kampuni ya uwekezaji kutoka nchini Uingereza ndio mwekezaji mkuu katika hatifungani hii na Balozi wa uingereza nchini, Mheshimiwa Marianne Young amesema CRDB Al Barakah Sukuk itaimarisha diplomasia ya kiuchumi kati ya Tanzania na Uingereza.
“Uingereza inajisikia fahari kushirikiana na Tanzania kuwezesha uwekezaji endelevu. Kupitia BII tunaiunga mkono Benki ya CRDB kutambulisha hatifungani ya kwanza isiyo na riba nchini. Mafanikio haya yanadhihirisha ushirikiano wetu wenye faida kwa pande zote mbili katika mkakati huu wa kufanikisha ukusanyaji paundi bilioni 1 kwa ajili ya uwekezaji mpaka mwaka 2030. Hii ni hatifungani kwanza ye Kiislamu ambayo BII imewekeza duniani na ni fuaraha kuona uwekezaji huo umefanyika Tanzania. Sukuk hii itatoa fursa ya uwezeshaji wa biashara zinazochangia kukua kwa uchumi,” amesema Mheshimiwa Marianne Young.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Sharia, Abdul Van Mohammed amesema imani ya dini ni kati ya vitu muhimu ambavyo huongoza uamuzi wa wawekezaji wengi.

“Hatifungani hii inafuata misingi ya Sharia lakini ipo kwa ajili ya kila Mtanzania. Tunamkaribisha kila mwekezaji aliye tayari kuwekeza katika CRDB Al Barakah Sukuk ili kwa Pamoja tuujenge Uchumi wetu,” amesema Mohammed.
Akieleza namna CRDB Al Barak Sukuk ilivyovutia macho ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, Mkurugenzi wa Uwekezaji wa BII, Jumai Mohammed amesema: “Tuna furaha kuwa mwekezaji mkuu wa CRDB Al Barakah Sukuk inayoendana na misingi yetu ya uwekezaji wezeshi na kukuza upatikanaji wa mitaji barani Afrika. Sukuk inadhihirisha umuhimu wa masoko ya mitaji na dhamana katika kukuza uchumi,” amesema Mohammed.
Afisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, CPA Nicodemus Mkama pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa dar es Salaam (DSE), Peter Nalitolela wamesema uzinduzi wa CRDB Al Barakah Sukuk unaonyesha kukua na kuimarika kwa masoko ya dhamana na mitaji nchini.

