Na Mwandishi wetu, Simanjiro
Mdau wa maendeleo wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara na Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha, Mula Sanare Sailepu Lesiangiki ametoa kiasi cha shilingi milioni 15 kama sehemu ya mchango wake wa kusaidia kampeni za uchaguzi wa wagombea wa Urais wa Chama Cha Mapinduzi CCM unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka 2025.
Mdau huyo wa maendeleo Mula Lesiangiki mbali ya kuchangia pia alikuwepo ukumbini hapo jana Agosti 12,2025, kushuhudia ‘LIVE’ hafla hiyo ya Harambee ikiendelea ndani ya ukumbi wa Mlimani City,jijini Dar es Salaam.
Harambee hiyo iliongozwa na Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan, ikilenga kukusanya kiasi cha fedha shilingi Bilioni 100 kwa ajili ya kampeni za uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Katibu Mkuu wa CCM na mgombea mwenza wa Urais kwa tiketi ya chama hicho Emmanuel John Nchimbi amesema katika harambee hiyo, CCM imefanikiwa kuchangisha kiasi cha fedha, jumla ya shilingi Bilioni 86.31 zikiwemo na ahadi, ambapo kuchangia huko kutafika tamati Agosti 27,2025.