BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekichukulia hatua za kisheria kiwanda bubu cha SUMING kilichopo Mtaa wa Regent Estate katika Kata ya Mikocheni wilayani Kinondoni kinachofanya shughuli za urejelezaji wa taka hatarishi aina ya simu za kiganjani chakavu katika eneo la makazi ya watu bila kibali cha kukusanya, kurejeleza, kuhifadhi na kusafirisha taka hizo jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira.
Zoezi hilo limefanyika mara baada ya timu ya wataalamu wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, TRA, pamoja na maafisa wa Serikali ya mtaa wa Regent kukagua kiwanda hicho na kubaini mapungufu yanayokiuka Sheria ya Usimamizi wa Mazingira nchini.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo Meneja Kanda ya Mashariki Kaskazini (NEMC) Bi. Glory Kombe amesema ni kosa kisheria kuanzisha kiwanda bila kusajili na kufuata taratibu za kimazingira ikiwepo kuzingatia ufanyaji wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na kupata vibali vya kukusanya na kurejeleza taka za kielectroniki. Ameutaka Uongozi wa Kiwanda hicho kufika mara moja Ofisi za NEMC ili waweze kupata taratibu zinazotakiwa kufuata wakati wa kuanzisha Mradi ili kuepuka madhara ya kimazingira na Afya ya viumbe hai.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule ameishukuru NEMC kwa kubaini na kukichukulia hatua Kiwanda hicho na amezitaka Taasisi zote zilizoshiriki ukaguzi wa Kiwanda hicho kuchukua hatua kwa mujibu wa Sheria na miongozo ya Taasisi husika.
Ameongeza kuwa Serikali imeweka Mazingira rafiki yanayovutia uwekezaji nchini hivyo wawekezaji watumie Mazingira hayo vizuri kwa kufuata utaratibu na Sheria ili kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa usalama, kuepusha uharibifu wa Mazingira na upotevu wa mapato ya Serikali.
Baraza linaendelea kutoa onyo kali kwa wawekezaji wote wanaoanzisha Viwanda bila kufuata taratibu (Viwanda bubu) ili kuepusha uharibifu wa Mazingira na kulinda Afya ya mazingira na viumbe hai.