Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi, ameridhishwa na ujenzi wa jengo jipya la utawala la Jiji la Arusha lenye ghorofa saba huku akitaka kuharakishwa kwa ujenzi huo ili likamilike kwa wakati.
Kihongosi akizungumza katika ziara hiyo ya kukagua maendeleo ya mradi huo pamoja na miradi mingine ya maendeleo jijini Arusha, Kihongosi amesema jengo hilo lina ubora wa hali ya juu na linagharimu shilingi bilioni 9.852, ambapo hadi sasa halmashauri imeshatoa shilingi bilioni 2.84 kupitia mapato ya ndani.
“Mradi una sifa zote za kuwa bora, kwa macho unaweza kuona quality ya ujenzi. Gharama za mradi zinaendana na ubora wake. Nayasema haya kwa sababu nimekagua miradi ya mwenge nchi nzima mwaka 2019. Unaona fedha imetumika vizuri sana, hongereni sana,” amesema Kihongosi.
Aidha alimtaka mkandarasi wa mradi huo, kampuni ya M/S Tribe Construction Ltd, kuhakikisha anatekeleza wajibu wake kwa ukamilifu na bila uzembe, akisisitiza kuwa muda wa nyongeza wa miezi mitatu walioomba baada ya tarehe ya awali ya kukamilika mwezi Septemba, uwe wa mwisho .
“Mkandarasi amenieleza kuwa structure inakamilika mwezi wa tisa lakini wameomba extension ya miezi mitatu. Nimemwambia Mkurugenzi hiyo iwe ya mwisho. Muanze kumkata anayozembea kuyatekeleza katika mradi. Jengo hili inabidi likamilike mwezi wa tano mwakani lianze kutumika,” ameongeza.
Kihongosi alimpongeza Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Kayombo, kwa usimamizi madhubuti wa mradi na kueleza matumaini yake kuwa jengo hilo litawezesha watumishi wote wa jiji kupata mazingira bora ya kufanyia kazi.
“Mkurugenzi Kayombo nakupongeza sana,najua kuna baadhi ya watumishi wanatumia majengo ya kata. Ujenzi huu ukikamilika watumishi wote wa jiji watapata nafasi. Nimesikia kwenye basement kuna sehemu ya kuegesha magari zaidi ya 100, hongereni sana,” amesema.
Kuhusu uchaguzi ujao, Kihongosi aliwahimiza watumishi na wananchi kushiriki kwa ufanisi na kuwachagua viongozi wazalendo, wachapakazi, wenye hofu ya Mungu na wanaoipenda nchi.
“Tunahitaji kumuunga mkono Mheshimiwa Rais. Mtumishi wa umma usiwe sehemu ya wanaoisema serikali, kwa sababu na wewe ni sehemu ya serikali. Tuieleze vizuri kwa kutekeleza wajibu wetu,” amesema.
“Kayombo, nakupongeza kwa kazi nzuri sana kuhakikisha Arusha inabadilika. Watumishi, naomba mumpe ushirikiano. Chini ya Mkuu wa Wilaya Mkude, Mkurugenzi Kayombo na watumishi, naamini lengo hili litafikiwa,” alihitimisha.
Jengo la utawala la Jiji la Arusha linatarajiwa kuwa miongoni mwa majengo ya kisasa ya halmashauri nchini na litasaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi pamoja na mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma.