Na John Bukuku – Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, Prof. Penina Mlama, ametangaza rasmi vigezo vya kushiriki katika duru ya nne ya tuzo hiyo kwa mwaka 2025/2026, yenye lengo la kukuza lugha ya Kiswahili na kuthamini mchango wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Agosti 13, 2025, jijini Dar es Salaam, Prof. Mlama amewataka waandishi bunifu kujitokeza kwa wingi kuwasilisha miswada yao, ambapo mapokezi yataanza Agosti 15, 2025, na kufungwa Novemba 30, 2025.
“Sasa vigezo tumeshavitaja. Ni wakati wenu waandishi bunifu kuwasilisha miswada yenu ili iweze kushindaniwa,” amesema Prof. Mlama.
Miongoni mwa vigezo vilivyotajwa ni pamoja na: mshiriki awe raia wa Tanzania; andiko bunifu liandikwe kwa lugha ya Kiswahili; sehemu yoyote ya mswada isiwe imewahi kuchapishwa na mchapishaji au kwa binafsi, ikiwemo kuchapishwa mtandaoni, magazetini, kurushwa kwenye vyombo vya habari na burudani au kuoneshwa jukwaani.
Vigezo vingine ni mwandishi kushiriki na andiko bunifu moja tu katika nyanja atakayochagua; mswada ulioshinda tuzo nyingine hautazingatiwa; na andiko bunifu liwe na ubora wa hali ya juu, likijikita katika masuala muhimu ya jamii. Aidha, miswada iliyoshika nafasi ya kwanza hadi ya kumi katika tuzo za miaka iliyopita haitaruhusiwa, lakini mwandishi anaweza kushiriki kwa kuwasilisha mswada mpya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), waandaaji wa tuzo hiyo, Dkt. Aneth Komba, amesema uanzishwaji wa tuzo hiyo umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la machapisho bunifu yenye maadili ya Kitanzania, ambayo sasa yanatumika na wanafunzi shuleni kama nyenzo za kujifunzia.
“Tunashukuru sana. Tuzo hizi zimekuza uandishi bunifu, na kwa sasa machapisho yameongezeka, yakibeba tamaduni za Kitanzania na kutumika shuleni. Hili ni jambo kubwa kwa uanzishwaji wa tuzo hii,” amesema Dkt. Komba.
Maadhimisho ya tuzo hiyo hufanyika kila Aprili 13, siku ya kuzaliwa kwa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye alifanya kazi kubwa ya kuenzi na kukuza lugha ya Kiswahili.