Benki ya Equity imezindua rasmi mfumo wa kidijitali unaoitwa “Shule Mkononi” (School in Your Hand), unaolenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu kwa taasisi za elimu na kuboresha huduma kwa wateja wake.
Kwa mujibu wa benki hiyo, mfumo huo utasaidia shule na vyuo kufuatilia taarifa za maendeleo ya kitaaluma ya wanafunzi, mahudhurio, na mapato ya shule kwa muda wowote, hivyo kuongeza ufanisi wa kiutawala na kifedha.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo Agosti 14, 2025 Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Huduma za Malipo wa Benki ya Equity, Christopher Msangule, alisema kuwa “Shule Mkononi” itarahisisha upatikanaji wa taarifa za kifedha, kitaaluma na kiutawala kwa ajili ya ukaguzi au tathmini.
“Mfumo huu utarahisisha ufuatiliaji wa ada, malipo na madeni kwa uwazi, jambo litakalowanufaisha wamiliki wa shule na vyuo,” alisema Msangule.
Aidha, alibainisha kuwa mfumo huo utaimarisha mawasiliano kati ya wazazi/walezi na taasisi za elimu, kwani utawawezesha kupata taarifa za maendeleo ya watoto wao moja kwa moja kupitia simu za mkononi, bila kulazimika kufika shuleni.
Mkuu wa Shule ya Awali na Msingi Moga, Henry Mungoli, aliipongeza Benki ya Equity kwa ubunifu huo, akieleza kuwa mbali na kurahisisha kazi za kiutawala, mfumo huo utaongeza usalama wa wanafunzi kwa kuwa na uwezo wa kurekodi na kufuatilia muda wa kuwasili shuleni.