Na Eleuteri Mangi, Dar es salaam
Wakazi wa Kivule jijini Dar es salaam wameipa kongole Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuwasogezea huduma karibu katika eneo hilo kwa kuendesha Kliniki ya Ardhi na kutoa Hatimiliki za Ardhi papo kwa papo.
Akizungumza na mwandishi wetu Agosti 14, 2025 jijini Dar es salaam, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dar es salaam Bi. Rehema Mwinuka amesema mwitikio wa wananchi wa kata ya Kivule ni mkubwa na watu wamehamasika kupata hati za maeneo wanayomiliki baada ya zoezi la ukwamuaji wa urasimishaji kukamilika.
Wakizungumzia namna wanavyopata huduma katika Kliniki hiyo, baadhi ya wananchi waliofika na kupata hati zao wamefurahishwa kwa ujio wa Kliniki hiyo Kivule kwa kuwa Serikali imewasogezea huduma za ardhi katika eneo lao, imewajali.
“Naishukuru Serikali kwa kutumilikisha ardhi na kutupatia hati, naipa kongole. Hati ina umuhimu, unatambulika na kuheshimika kwenye ardhi uliyonayo, hata serikali itakapohitaji ardhi hiyo kwa matumizi mengine, haitakuwa sawa na ardhi ambayo haijamilikishwa, hati itakulinda katika masilahi mengi” amesema Mohamed Ramadhan Athumani mkazi wa Kivule.
Aidha, katika Kliniki hiyo, zipo pia huduma nyingine zinazotolewa ikiwemo uhakiki na utambuzi wa viwanja vya wananchi katika maeneo yao, kupata namba ya malipo kulipia kodi ya pango la ardhi, (control number), kupokea, kusikiliza na kutatua migogoro mbalimbali ya ardhi.
Kliniki hiyo Maalum ya Ardhi ambayo inaendeshwa na Wizara, inafanyika katika mikoa ya Dar es Salaam katika Manispaa ya Ilala, Dodoma eneo la Mpunguzi, Mbeya halmashauri ya Mbarali na Shinyanga katika halmashauri ya Kahama pamoja na Manispaa ya Shinyanga.