Na Mwamvua Mwinyi,Mafia
Agost 15,2025
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Petro Magoti amesisitiza kufanya kazi kwa bidii na kujituma hususan katika usimamizi wa Miradi ya Maendeleo ili iweze kuleta tija na kuunga juhudi za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan katika kukuza Maendeleo.
Magoti ameyasema hayo akiwa katika ziara ya Katibu Tawala Mkoa wa Pwani ,Pili Mnyema katika kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.
Aidha amesema kuanzia jumamosi atarudi tena Wilayani hapo ili kuangalia maendeleo ya miradi inayokamilishwa na kufuatilia utekelezaji wa maelekezo yalitolewa na Katibu Tawala.
“Hatucheki na Mtu kwenye Miradi, kuanzia jumamosi nitakuwa hapa kuhakikisha mambo yote yaliyoanishwa yanatekelezwa,” alisema Magoti.
Wilayani Mafia Katibu Tawala alikagua mradi wa ujenzi wa soko la Kilindoni unaogharimu zaidi ya Milioni 700, Ujenzi wa Jengo la wazazi kakika Hospitali ya Wilaya unaogharimu zaidi ya milioni 500 pamoja na Maboresho ya majengo ya Shule ya Msingi Utende yanayogharimu zaidi ya sh. Milioni 100.