

Mtunzi na mwimbaji wa nyimbo mbalimbali za hamasa za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akiwemo wimbo maarufu “Tundu Lissu Wapeleke Mchakamchaka”, George Mwingira amefariki dunia baada ya kupata ajali ya gari.
Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kusini, Belle Ponera, Mwingira alifariki dunia Jumapili, Agosti 10, 2025, katika eneo la Mikumi, mkoani Morogoro, baada ya basi alilokuwa akipanda kutoka Songea (Ruvuma) kuelekea Dar es Salaam kupata ajali.
Mbali na wimbo huo, Mwingira maarufu kama MC Mwingira aliwahi pia kutamba na kibao cha “No Reforms No Election”, ambacho ndicho kilikuwa kazi yake ya mwisho kabla ya kifo chake.
Kifo chake kimeendelea kuwa pigo kwa CHADEMA kwa kuwapoteza wasanii wake wa nyimbo za hamasa, ambapo kabla yake walifariki dunia:
Fulgence Mapunda ‘Mwanacotide’ (2019), aliyeimba “Chadema People’s Power” na “Polisi Msitupige Mabomu Chadema”.
Sara Alex (2022), aliyeimba wimbo “Mwamba Tuvushe”.