FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Mkuu wa Chuo cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Mheshimiwa Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba, amesema chuo hicho kinawajibika kuhakikisha kinawasaidia wananchi, hasa wakulima na wafugaji, kuondokana na umaskini kupitia kilimo na mifugo, kutokana na umuhimu wake kitaifa na kimataifa.
Jaji Warioba aliyasema hayo wakati wa hafla ya kuzindua Baraza jipya la Kumi na Nne la Chuo hicho, sambamba na kuaga na kutoa zawadi kwa Baraza la Kumi na Tatu lililokuwa likiongozwa na Mwenyekiti, Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman, kwa kipindi cha miaka mitatu.
Katika hotuba yake, Jaji Warioba alisema kuwa bila SUA hakuna namna wananchi, hasa wakulima na wafugaji, wanaweza kuondokana na umaskini, kwa sababu asilimia kubwa ya Watanzania wanategemea kilimo na mifugo.
“Hakuna njia nyingine ya kuwafanya wakulima na wafugaji kuondokana na umaskini kama SUA itashindwa kuwasaidia kama inavyofanya sasa. Tangu kuanzishwa kwake, chuo hiki kimeleta mabadiliko makubwa kutokana na tafiti mbalimbali zinazofanywa na wataalamu wenye weledi,” alisema Jaji Warioba.
Aidha, aliongeza kuwa mabadiliko hayo yamechagizwa na menejimenti imara ya chuo na baraza lililodhamiria kuhakikisha Watanzania, hasa wakulima na wafugaji, wanapata huduma bora zenye manufaa.
“Ninaongea haya kwa dhati kabisa kuwa Mheshimiwa Jaji Chande, baraza lako limefanya kazi kubwa ya kukibadilisha chuo hiki. Matarajio yangu kwa baraza hili jipya ni kuona mkifanya kazi kubwa zaidi kukisaidia chuo kupiga hatua mbele,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kumi na Tatu, Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman, alishukuru kwa ushirikiano mkubwa alioupata wakati wa uongozi wake na kuwataka wajumbe wapya kuongeza kasi katika kukiendeleza chuo.
Awali, Makamu Mkuu wa Chuo cha SUA, Profesa Rafael Chibunda, alisema kuwa uwepo wa baraza umechochea maendeleo na kasi ya ukuaji wa chuo katika masuala ya utafiti, teknolojia na ushauri wa kitaalamu.