Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke limefanikiwa kuwakamata wafanyabiashara wanne wa Soko la Mbagala Rangi Tatu kwa tuhuma za kujiunganishia nishati ya umeme kinyume cha taratibu, kwa kutumia mafundi wasio rasmi maarufu kama “vishoka”.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika Operesheni Maalum ya kuwasaka na kuwachukulia hatua watu wanaohusika na uharibifu wa miundombinu ya umeme, Fundi Sanifu wa Umeme kutoka Idara ya Udhibiti Mapato TANESCO Mkoa wa Temeke, Bw. Yasini Bakari, amesema kuwa watuhumiwa wote tayari wamefikishwa katika vyombo vya dola kwa ajili ya hatua za kisheria.
Bw. Bakari amesema kuwa operesheni hiyo inalenga kukomesha vitendo vya baadhi ya wananchi wanaotumia nishati ya umeme kwa njia zisizo halali bila kulipia, jambo linalosababisha hasara kubwa kwa shirika.
Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kutumia huduma rasmi za TANESCO ili kuomba umeme kwa njia salama, rahisi na ya haraka, badala ya kutumia njia haramu zinazoweza kuhatarisha maisha na mali zao.
TANESCO Mkoa wa Temeke imeahidi kuendelea na operesheni hiyo katika Mkoa huo hadi pale vitendo vya hujuma na wizi wa umeme vitakapokwisha.