Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
CHAMA cha United,Democratics Party,(UDP) kimesema kama kitapewa ridhaa ya kushika dola kitawajaza watanzania fedha ili waweze kujikomboa kiuchumi,huku wakikisisitiza suala la haki za wanawake katika uongozi ikiwemo kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Hayo yamesemwa leo Agosti 15,2025 na mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama hicho,Saum Hussein Rashid wakati akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma,mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea urais katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) iliopo Njedengwa Dodoma
Saum akiwa na mgombea mwenza,Juma Khamisi Faki,amesema watawajaza fedha watanzania kwa kufungua fursa mbalimbali katika sekta za kilimo,kuboresha miundombinu pamoja na kuongeza idadi ya wataalamu katika sekta ya elimu.
“Tunaposema kuwajaza fedha watanzania tuna maana ni kuweka miundombinu mizuri kwa wananchi ili waweze kupata fedha ambazo zitawainua kiuchumi kwa mfano zao la Pamba walime kisasa na mazao mengine.
Amesema pia ni kuboresha ile miundombinu ya watu kuwa na fedha kwa sababu atafanya kilimo chenye tija ndio maana tunasema kuwajaza fedha ni kufungua fursa zinazopelekea biashara kufanyika.
Kuhusu suala la haki ya wanawake katika uongozi amesema UDP itahakikisha wanawake wanaingia katika uongozi na kuongeza watatokomeza pia ukatili wa kijinsia.
