▪️Waziri Mavunde azindua Kiwanda cha kuongeza thamani madini Chumvi-Kigoma
▪️Ni cha uzalishaji Chumvi Lishe(𝐶𝑎𝑡𝑡𝑙𝑒 𝐿𝑖𝑐𝑘) kwa ajili ya Mifugo
▪️Lengo ni kupunguza uagizaji wa Chumvi Lishe kutoka nje ya Nchi
▪️Tanzania kuongeza uzalishaji wa Chumvi ghafi kwa matumizi ya viwandani
Uvinza,Kigoma
Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Nyanza Salt kwa kuitikia wito wa Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan wa uongezaji thamani madini nchini kwa kuanza rasmi uzalishaji wa chumvi lishe itokanayo na madini ya Chumvi mahususi kwa ajili ya kuongeza virutubisho vya mifugo.
Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Wilayani Uvinza-Kigoma wakati akizindua shughuli za Kiwanda cha kuzalisha chumvi lishe(𝘾𝙖𝙩𝙩𝙡𝙚 𝙇𝙞𝙘𝙠) kwa ajili ya mifugo kinachomilikiwa na Kampuni ya Nyanza Salt.
“Ni wito wa Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan na matakwa ya sheria juu ya uongezaji thamani madini yetu hapa nchini.
Nawapongeza Kampuni ya Nyanza kwa hatua hii kubwa ya kuitoa chumvi yetu katika matumizi ya kawaida na kuiongezea thamani kuzalisha Chumvi lishe ambayo ni muhimu kwa virutubisho vya mifugo.
Wafugaji wengi huagiza chumvi lishe kutoka nje ya nchi kwakuwa hakukuwa na uzalishaji hapa nchini,hatua hii ya leo ya uzalishaji wa 𝘾𝙖𝙩𝙩𝙡𝙚 𝙇𝙞𝙘𝙠 nchini itapunguza uagizwaji wa bidhaa hii kutoka nje ya nchi kwa kiwango kikubwa hivyo natoa rai kwa wafugaji kuiunga mkono bidhaa hii inayozalishwa ndani ya ya nchi.
Tasnia ya chumvi inaendelea kukua kwa kasi siku hadi siku na lengo la serikali ni kuhakikisha tunaboresha mazingira ya uwekezaji kwenye eneo hili ili kuongeza tija na uzalishaji na kuondokana kabisa na uagizaji wa chumvi ghafi kutoka nje ya nchi kama malighafi ya viwanda” Alisema Mavunde
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Nyanza Salt Mines Ndg. Mukesh Mamlani amesema uzalishaji wa bidhaa ya chumvi lishe itokanayo na madini chumvi ni mkombozi kwa wafugaji wa Tanzania na kwamba kampuni itahakikisha inakidhi viwango na ubora wa bidhaa ili wafugaji wa Tanzania wanufaike.
Pia Ndg. Mukeshi ameeleza kwamba mpango wa Kampuni ni uzalishaji wa tani 120,000 za chumvi ifikapo mwaka 2027 ili kuhakikisha chumvi ya kutosha inapatikana nchini.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Uvinza,Mh. Dina Mathamani amesema uwepo wa Kampuni ya Nyanza wilayani Uvinza umekuwa ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi na mapato kwa serikali na wananchi ambapo kupitia Ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja jumla ya wa wananchi 1000 wamekuwa wakipata Ajira kiwandani hapo wakati wa msimu wa uchakataji chumvi.