*Awanoa Wanawawake na Wajasiriamali Songwe kuhusu Nishati Safi ya Kupikia
*Atoa wito kwa Wadau kushirikiana na Wizara ya Nishati kutoa elimu ya Nishati Safi ya Kupikia
Songwe
Imeelezwa kuwa matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia si tu yanahatarisha afya bali pia yanachochea uharibifu wa mazingira ambapo takribani hekta 400,000 za misitu hupotea kila mwaka nchini kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa, jambo linalochangia kuongezeka kwa ukame na mabadiliko ya tabianchi.
Hivyo, Watanzania wameaswa kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuachana na matumizi ya nishati isiyo safi kama kuni na mkaa kutokana na athari zake kwa binadamu na mazingira.
Wito huo umetolewa leo Agosti 16, 2025, na Mjiolojia kutoka Wizara ya Nishati, Nsajigwa Maclean, wakati akitoa elimu ya Nishati Safi ya Kupikia kwa Wajasiriamali mkoani Songwe.
Amesema kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, ni asilimia 16 tu ya Watanzania ndio wanaotumia nishati safi ya kupikia, hivyo bado kuna magonjwa yanayotokana na moshi wa kuni na mkaa, ambayo yanasababisha vifo vya zaidi ya watu 33,000 kwa mwaka nchini.
Katika ngazi ya kimataifa, amesema watu bilioni 2.1 hawana upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, huku zaidi ya watu milioni 3 wakifariki dunia kila mwaka kutokana na madhara ya kiafya yanayotokana na nishati isiyo safi ya kupikia ambapo Kusini mwa Jangwa la Sahara zaidi ya watu milioni 960 hawana nishati hiyo.
Aidha amebainisha kuwa kuna dhana potofu miongoni mwa jamii kuwa chakula kinachopikwa kwa kutumia gesi au umeme hakiwi na ladha nzuri, jambo ambalo amesema halina msingi wa kisayansi na linaendelea kuwazuia wananchi wengi kufanya mabadiliko kuelekea matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Ameeleza kuwa Wizara ya Nishati imeweka mkakati wa kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ili kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia, huku mkakati huo ukiangazia mafanikio kutoka nchi nyingine kama India na Ghana, ambazo zimepiga hatua katika kuhimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Imeelezwa pia kuwa changamoto kubwa kwa wananchi si kutotaka kutumia nishati safi ya kupikia bali wanahitaji elimu pia kuhusu matumizi ya nishati hiyo hivyo ametoa wito kwa Wadau kushirikiana na Serikali katika kutekeleza Mkakati wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia.
Katika semina hiyo wanawake na wajasiriamali walihimizwa kuwa mabalozi wa mabadiliko kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia si kwa ajili ya afya pekee, bali pia kwa ajili ya kulinda mazingira na kizazi kijacho.