
Kigali, Rwanda – Wananchi Young Africans SC wameharibu sherehe ya Rayon Sports Day baada ya kuichapa wenyeji wao Rayon Sports mabao 3-1 katika uwanja wa Amahoro na kutwaa kombe la Rayon Day Cup 2025.
Rayon walipata goli la mapema dakika ya kwanza kufuatia Andambwile kujifunga na kuwapa mashabiki wa nyumbani matumaini ya ushindi. Hata hivyo, Yanga SC walionyesha ubabe wao baadaye kwenye mchezo.
Bao la kusawazisha liliwekwa kimiani dakika ya 27 na Maxi Boyeli, kabla ya Stephane Aziz Ki “Pacome” kufunga dakika ya 44 na kuwapeleka Yanga mapumziko wakiwa mbele kwa 2-1.
Mchezo ulionekana kuisha kwa matokeo hayo, lakini dakika za nyongeza (90+2) Bakari Mwamnyeto aliihakikishia Yanga ushindi mnono kwa kufunga bao la tatu.
Kwa matokeo haya, Yanga SC wametibua sherehe za Rayon Sports na kuondoka Kigali wakiwa na kombe la kihistoria cha Rayon Day Cup 2025.
FT: Rayon Sports 1-3 Yanga SC
Magoli:
Rayon Sports: Andambwile (dakika ya 01, OG)
Yanga SC: Boyeli (27’), Pacome (44’), Mwamnyeto (90+2’)