Dar es Salaam, 17 Agosti 2025 – Maelfu ya wakimbiaji na wapenda michezo kutoka ndani na nje ya Tanzania wamejitokeza leo katika viwanja vya The Green, Oysterbay, kushiriki CRDB Bank Marathon 2025, mbio za hisani ambazo mwaka huu zimekusanya Shilingi Bilioni 2 ili kusaidia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo, wakinamama wenye ujauzito hatarishi, na vijana kupitia programu ya iMBEJU.

Akitoa salamu zake, Dkt. Tulia alipongeza ubunifu wa CRDB Bank Foundation katika kuunganisha jamii kupitia michezo na kusaidia wenye uhitaji, akieleza kuwa mbio hizo ni mfano wa vitendo vya huruma vinavyogusa maisha ya wengi.
Akitoa salamu zake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, aliipongeza Benki ya CRDB na CRDB Bank Foundation kuendelea kuandaa mbio hizo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alibainisha kuwa msimu wa sita wa CRDB Bank Marathon umefanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 30 ya Benki ya CRDB, na kuendelea kupanua wigo wa matokeo yake ndani na nje ya Tanzania. Kwa mara ya pili, mbio hizi zimefanyika pia nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), zikikusanya fedha kwa ajili ya miradi ya afya na ustawi wa jamii katika nchi hizo.
Nsekela alisema kuwa mbio za mwaka huu zimeweza kuvutia zaidi ya washiriki 16,000, na kufanikisha lengo la kukusanya shilingi bilioni 2 ambapo pamoja na kusaidia maandalizi ya mbio hizo, shilingi milioni 450, zimeelekezwa kusaidia wenye uhitaji katika jamii.
Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya mbio hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, alieleza kuwa safari ya msimu wa sita imeanzia Lubumbashi, DRC, ambako zilikusanywa Dola za Marekani 70,000 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika hospitali ya Jeshi la Ruashi, na kuendelea Bujumbura, Burundi, ambapo zilipatikana Faranga za Burundi milioni 175 kusaidia bima ya afya kwa zaidi ya watu 58,000 wasiojiweza.
CRDB Bank Marathon imekuwa jukwaa muhimu la kuchochea ustawi wa kijamii katika ukanda huu wa Afrika ya Mashariki na kati hivi karibuni ikipata heshima ya kutambuliwa kimataifa kwa kushinda tuzo ya jukwaa bora la taasisi za fedha katika kusaidia kusaidia jamii.