Idadi ya mafundi waliookolewa baada ya kufunikwa na kifusi mgodini imefikia saba, baada ya Marko Ngelela (26), mkazi wa Sengerema na Machia Shabani (43) mkazi wa Ishokela mkoani Mwanza kuokolewa wakiwa tayari wamefariki dunia.
Ajali hiyo ilitokea Agosti 11, 2025 katika mgodi wa Nyandolwa, wakati mafundi 25 walipokuwa wakifanya kazi ya ukarabati katika maduara matatu tofauti ambayo ni Na. 20, 103 na 106. Kwa mujibu wa taarifa za awali, ardhi ilititia ghafla na kusababisha kifusi kuporomoka, hali iliyowafunika baadhi ya mafundi waliokuwa kazini chini ya ardhi.
Tangu tukio hilo kutokea, juhudi kubwa zimekuwa zikiendelea kutoka kwa timu ya uokoaji ya mgodi huo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, pamoja na wataalamu wa usalama wa migodini. Hadi sasa, mafundi saba wamefanikiwa kutolewa chini ya kifusi, ambapo wanne kati yao waliokolewa wakiwa hai ambapo mmoja kati yao alifariki wakati akipatiwa matibabu katika Kituo cha Afya cha Salawe na watatu walitoka wakiwa tayari wamepoteza maisha.
Hali ya mafundi wengine 18 waliobaki chini ya ardhi bado haijafahamika, huku juhudi za kuwaokoa zikiendelea kwa uangalifu mkubwa ili kuepuka majanga zaidi kutokana na mazingira magumu na hatarishi ndani ya mgodi huo.
Mamlaka husika zimetoa wito kwa wananchi kuwa watulivu wakati juhudi za uokoaji zikiendelea, huku wakiahidi kufanya kila linalowezekana kuhakikisha maisha ya waliobaki yanaokolewa.