Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Ivato, kushiriki Mkutano wa 45 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika Antananarivo nchini Madagascar leo tarehe 17 Agosti 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Rais wa Afrika Kusini Mhe. Cyril Ramaphosa wakati alipowasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Ivato, kushiriki Mkutano wa 45 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika Antananarivo nchini Madagascar leo tarehe 17 Agosti 2025. (Katikati ni Rais wa Botswana Mhe. Duma Boko)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kabla ya kuanza kwa Mkutano wa 45 wa SADC unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Ivato, Antananarivo nchini Madagascar leo tarehe 17 Agosti 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akishiriki Mkutano wa 45 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Ivato, Antananarivo nchini Madagascar leo tarehe 17 Agosti 2025.
Matukio mbalimbali wakati wa Mkutano wa 45 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Ivato, Antananarivo nchini Madagascar leo tarehe 17 Agosti 2025.
…………
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 45 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Ivato, Antananarivo nchini Madagascar.
Katika Mkutano huo Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe Mhe. Emmerson Mnangagwa amekabidhi Uenyekiti wa SADC kwa Rais wa Jamhuri ya Madagascar Mhe. Andry Nirina Rajoelina utakaodumu kwa kipindi cha mwaka mmoja. Vilevile Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekabidhi uenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama (SADC Organ Troika) kwa Jamhuri ya Malawi mara baada ya kuhitimisha uongozi wa mwaka mmoja wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ulioanza Agosti 2024.
Akisoma hotuba ya ufunguzi Mwenyekiti wa SADC anayemaliza muda wake, Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe Mhe. Emmerson Mnangagwa pamoja na mambo mengine amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiongoza vema Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama na kuhakikisha amani na utulivu katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika.
Mkutano huo umejadili hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Mpango Mkakati Elekezi wa kanda, kuanisha mafanikio na changamoto za utekelezaji. Utekelezaji umejikita katika nguzo kuu nne zikiongozwa na nguzo kuu ya Amani, Usalama na Utawala wa Kidemokrasia. Nguzo nyingine ni maendeleo ya viwanda na utangamano wa masoko, Maendeleo ya miundombinu katika kuchagiza utangamano pamoja na maendeleo ya kijamii na rasilimali watu.
Miongoni mwa mafanikio yaliyojadiliwa ambayo yamepatikana ni pamoja na kupungua kwa matukio ya ugaidi, kuimarika kwa demokrasia katika Kanda kupitia chaguzi huru na haki, kuongezeka kwa huduma za kifedha, kuongezeka kwa thamani ya mauzo ya bidhaa za viwanda na kuongezeka kwa miamala iliyofanyika kupitia mfumo wa malipo wa kikanda (Real Time Gross Settlement – RTGS).
Katika Mkutano huo washindi mbalimbali wa Tuzo zinazotolewa na SADC wametangazwa ikiwemo Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari kutoka nchini Tanzania Crispin Kamugisha aliyetangazwa mshindi katika uandishi wa insha na kuzawadiwa dola elfu moja mia tano.
Kauli mbiu ya Mkutano wa 45 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ni “Kuendeleza Viwanda, Mageuzi ya Kilimo na Matumizi bora ya Nishati kwa ustahimilivu wa kanda ya SADC” (Advancing Industrialisation, Agricultural Transformation, and Energy Transition for a Resilient SADC).