Mwandishi Wetu
Morogoro
Benki ya NMB imeahidi kuendelea kutoa elimu ya fedha nchini ili kuzuia wananchi kuingia hasara kutokana na kuhifadhi fedha sehemu zisizo salama, ikiwemo kuzifukia ardhini, kuzihifadhi chini ya godoro au ndani ya nyumba.
Akizungumza katika tamasha la NMB Kijiji Day lililofanyika Misongeni, Manispaa ya Morogoro, Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Janeth Shango, alisema benki hiyo itaendelea kubuni mbinu zaidi za kupeleka elimu ya kifedha moja kwa moja vijijini. Hatua hii inalenga kuondoa changamoto ya wananchi wengi kukosa huduma za kibenki kutokana na umbali na ukosefu wa miundombinu.
Janeth aliongeza kuwa kupitia NMB Kijiji Day, benki itawafuata wananchi vijijini kwa kushirikiana nao katika michezo, kuwapatia elimu ya fedha, na kushiriki nao chakula, huku ikiendelea kuwapatia masuluhisho ya kifedha. Hii itawasaidia wananchi kujua njia sahihi za kutunza fedha kwa usalama zaidi na kuachana na mbinu zisizo salama.
“NMB imekuwa ikifanya utafiti wa kutatua changamoto za sekta ya fedha kwa kutoa elimu zaidi kwa wananchi waliopo vijijini. Utafiti wetu umebaini baadhi ya wananchi hutunza fedha sehemu zisizo salama na wamekuwa wakipoteza fedha kutokana na njia hizo. Hali hii imesababisha benki kuimarisha kampeni za utoaji elimu kwa kuwafuata watu vijijini,” alisema Janeth.
Aidha, Janeth alisema jitihada hizo zimeifanya NMB kuendelea kutambuliwa kimataifa, ambapo jarida la Euromoney katika ripoti ya 2025 limeitaja benki hiyo kuwa kinara katika uwajibikaji wa kijamii, hususan katika mazingira, jamii na utawala bora.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Msingi wa Manispaa ya Morogoro, Gregory Mtalemwa, aliipongeza NMB kwa mchango wake katika maendeleo ya kijamii.
“Kampeni yenu ya NMB Kijiji Day imewakutanisha wananchi wengi kupitia michezo na burudani, lakini kubwa zaidi ni elimu ya kifedha mnayotoa. Pia tumeona msaada wenu wa madawati 50 yenye thamani ya Sh milioni 5 kwa Shule ya Msingi Misongeni, jambo linaloonyesha mshikamano wenu na jamii,” alisema Mtalemwa.
Naye Kaimu Mtendaji wa Kata ya Bigwa, Fatuma Suleiman, alisema NMB imeendelea kufikisha huduma kwa wananchi wa kata hiyo yenye mitaa 13, sambamba na kuunga mkono jitihada za serikali katika uhifadhi wa mazingira kupitia upandaji miti.
Tamasha hilo la NMB Kijiji Day limeonekana kuwa chachu ya mshikamano wa kijamii, kukuza maendeleo ya ndani, na kuchochea afya na ustawi wa jamii kupitia michezo, elimu na burudani.