Na mwandishi wetu, Simiyu
Wafanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu wameiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoa elimu ya kodi mara kwa mara ili kila mwananchi afahamu umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa.
Wakizungumza wakati wa semina ya mabadiliko ya sheria za kodi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 iliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya TRA mkoani Simuyu, wafanyabiashara hao wamesema kuwa, elimu ya kodi ikitolewa kila mara, itasaidia watu kujua faida za kodi na hivyo kupunguza vitendo vya ukwepaji kodi.
“Tunaomba elimu hii iendelee kutolewa mara kwa mara, yapo makundi mengi leo hii hayajapata elimu hii, tunawaomba TRA iwafikie na wao, hii itapunguza kwa kiwango kikubwa watu kukwepa kodi na kujua umuhimu wa kulipa kodi,” alisema Bw. Elias Nungwana.
Bw. Mbowe Malemi ambaye ni mfanyabiashara wa Bariadi mjini mkoani humo, ameishukuru TRA kwa kuwapa elimu ya mabadiliko ya sheria hizo, na kueleza kuwa, sheria mpya nyingi ambazo zimebadilishwa ni rafiki kwao na zitawasaidia katika kuongeza mwamko wa kulipa kodi.
“Tunawashukuru sana TRA kwa huu utaratibu, kila mwaka tumeanza kuona wanakuja kutupa elimu jambo hili linatufanya tulipe kodi kwa hiari kwani tunakuwa na uelewa wa sheria mpya na zile za zamani,” alisema Bw. Malemi.
Kwa upande wake Meneja Msaidizi wa TRA Mkoa wa Simiyu Bw. Honest Mushi alisema kwamba, kutolewa kwa elimu hiyo kwa walipakodi mkoani humo, itasaidia Mamlaka hiyo kufikia lengo la mkoa ambalo ni shilingi bilioni 30.4 katika mwaka huu wa fedha 2025/2026.
Meneja Msaidizi huyo alisema kuwa, walipakodi katika mkoa huo wamekuwa wakitoa ushirikiano mkubwa kwa Mamlaka hiyo, hali ambayo imewezesha kuvuka lengo kwa kukusanya zaidi ya asilimia 100 katika mwaka wa fedha uliopita wa 2024/2025.
Naye, Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi kutoka TRA Bi. Eugenia Mkumbo alisema lengo la elimu hiyo ni kuwawezesha walipakodi kutambua na kuelewa wajibu wao katika suala zima la ulipaji kodi kwa hiari.
“Tunawaomba walipakodi wote kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kama inavyoelekezwa kwenye sheria za kodi, baada ya elimu hii kila mmoja awe ametambua wajibu wake na kwa muda gani anatakiwa kulipa kodi,” alisema Bi. Eugenia.
Timu ya maafisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania inapita katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kutoa elimu ya mabadiliko ya sheria za kodi yaliyotokea mara baada ya kupitishwa kwa Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2025/2026.

Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bi. Eugenia Mkumbo akiwasilisha mada ya mabadiliko ya sheria za kodi kwa mwaka wa fedha 2025/26 katika semina ya wafanyabiashara iliyofanyika iliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya TRA mkoani Simiyu.

Baadhi ya Walipakodi waliohudhuria semina ya mabadiliko ya sheria za kodi kwa mwaka wa fedha 2025/26 wakifuatilia kwa makini semina hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya TRA mkoani Simiyu.

Baadhi ya Walipakodi waliohudhuria semina ya mabadiliko ya sheria za kodi kwa mwaka wa fedha 2025/26 wakifuatilia kwa makini semina hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya TRA mkoani Simiyu

Mshauri wa Kodi kutoka Kampuni ya Finx Capital House Bw. Jackson Samwel akitoa maoni yake wakati wa semina ya wafanyabiashara kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 iliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya TRA mkoani Simiyu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bariadi Education Centre Limited Bi. Elizabeth Yuma akichangia hoja wakati wa semina ya wafanyabiashara kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 iliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya TRA mkoani Simiyu.
