Polisi kata ya Isongole Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Felix Cedrick, amewaelimisha na kuhamasisha wananchi hususani wafanyabiashara na wanunuzi wa bidhaa katika Soko la Isongole Wilaya ya Ileje Mkoa wa Songwe, kuhusu masuala muhimu yanayohusu usalama wao na mustakabali wa taifa.
Elimu hiyo ameitoa Agosti 17, 2025 katika soko hilo na alisema katika nyakati za sasa ambapo teknolojia imekuwa sehemu ya maisha ya kila siku, matukio ya wizi wa mtandaoni (wizi kwa njia ya kidigitali) yamekuwa yakiongezeka hivyo nawaomba muwe na tahadhari na umakini wa hali ya juu kwa mawakala wasio rasmi wa miamala ya kifedha wanaozurura hovyo katika maeneo ya masoko na mitaani.
“Niwaombe wananchi na kuwahimiza wafanyabiashara kuepuka kutumia huduma za fedha kutoka kwa watu wanaojitambulisha kama mawakala bila kuwa na ofisi rasmi au vitambulisho vinavyotambulika kisheria, badala yake tumieni ofisi halali za mawakala wa mitandao ya kifedha ambazo zinatambulika na zimesajiliwa kisheria” alisema Mkaguzi Felix.
Mkaguzi Felix aliendelea kuwasisitiza wafanyabiashara hao kuwa waangalifu na wale wanaodai kuwasaidia katika miamala ya simu bila idhini, kwani baadhi yao hutumia ujanja huo kuwaibia wananchi.
Pamoja na elimu hiyo, Mkaguzi Felix aliwakumbusha wananchi hao kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, na kuwataka wananchi wote wa Isongole na maeneo jirani kujiandaa na kufuatilia kwa amani shughuli zote za kampeni za wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi – Rais, Wabunge na Madiwani.
“Wananchi wanapaswa kudumisha utulivu, kuheshimu maoni ya wengine, na kujiepusha na vitendo vya uchochezi au vurugu vinavyoweza kuvuruga amani ya taifa letu, kila mmoja anao wajibu wa kulinda amani kwa kushiriki uchaguzi kwa njia ya kidemokrasia na kistaarabu” alisema Mkaguzi Felix.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linaendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha kuwa usalama unadumishwa wakati wote wa kampeni, uchaguzi na baada ya uchaguzi, na aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa haraka juu ya viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani au uhalifu katika maeneo yao ili vishughulikiwe kwa mujibu wa sheria ikiwa kushirikiana na kudumisha amani na usalama kwa Maendeleo ya Taifa.