Wakulima wanaojihusisha na kilimo cha tumbaku kupitia chama cha msingi Namkeke wamepata mafanikio makubwa kiuchumi kufuatia ushirikiano na kampuni ya 3H.TOBACCO LTD Kampuni hiyo imenunua tumbaku ya wakulima hao kwa bei nzuri na kuhakikisha malipo yote yanafanyika kwa wakati, jambo lililowapa wakulima motisha na matumaini makubwa katika shughuli zao za kilimo.
Katika mahojiano na baadhi ya wakulima, wengi walieleza kuwa kwa mara ya kwanza wameweza kupata faida halisi kutokana na kilimo chao.
Abdallah Ndine ni Mkulima wa Tumbaku kijiji cha Litola amesema, Malipo ya haraka na yenye uwazi kutoka kampuni ya 3H Tobacco LTd yamewasaidia kulipa madeni ya pembejeo, kugharamia elimu ya watoto na hata kuanzisha miradi midogo ya kiuchumi kama ufugaji na biashara ndogo ndogo. Hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kuinua hali zao za maisha.
Mwenyekiti Chama cha msingi Namkeke kilichopo Namtumbo Cathberth Nyoni ameripoti ongezeko la wanachama wapya,zaidi ya 100 huku wengi wakivutiwa na mafanikio yanayoonekana.
Aidha , Viongozi wa chama wameeleza kuwa ushirikiano na kampuni ya 3H Tobacco umeleta mageuzi makubwa, na sasa wana mpango wa kupanua mashamba ya tumbaku pamoja na kuwajengea wakulima uwezo wa kutumia mbinu bora zaidi za kilimo.
Katika kuhakikisha maendeleo hayo yanaendelezwa, chama kwa kushirikiana na Kampuni ya 3H Tobacco kimeweka mikakati thabiti ikiwemo kutoa mafunzo ya kilimo bora, kuanzisha vikundi vya kuweka na kukopa kwa wakulima, pamoja na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa mazao. Lengo ni kuhakikisha wakulima wanazidi kupata faida na kuondokana na utegemezi wa misaada ya nje.
Naye Mkulima Hamza Issa akizungumza kwa niaba ya Wakulima wenzie ametoa shukrani kwa kampuni ya 3H Tobacco kwa kuwa mshirika mwaminifu wa maendeleo na wametoa wito kwa kampuni hiyo kuendelea kushirikiana nao kwa miaka mingi ijayo.
Kwa sasa, matumaini ni makubwa na wakulima wengi wanaamini kuwa kupitia ushirikiano huu, wanaweza kufikia mafanikio ya kiuchumi ya kudumu.
kwa upande wake Meneja wa kampuni hiyo Issa Ponera amesema kampuni yao itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wakulima kwa kuwakopesha pembejeo, kuwapatia ushirikiano , kulipa kwa wakati na kuwasafirishia tumbaku yao toka mashambani ambapo amewataka wakulima watumie kampuni hiyo kwani ni mkombozi wao.
Viongozi wa kampuni ya 3H Tobacco LTD wakiwa na Mkulima wa tumbaku Abdallah Ndine baada ya kumkabidhi usafiri wa Bodaboda imsaidie kwenye shuguli zake za kilimo hali ambayo imewagamasisha wakulima wengi waliokata tamaa kurudi shambani msimu 2025/2026