………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza leo Agosti 18,2025, limemfikisha katika Mahakamani ya wilaya ya Ilemela Kulwa Steven Ibasa (maarufu kama Baba Claud), mwenye umri wa miaka 37 na mkazi wa Nyakato kwa tuhuma za kumlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka minne (jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kisheria).
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa na Wakili wa Serikali Mwanahawa Changali mbele hakimu mkazi Mwandamizi Mhe, Juma Opudo, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo tarehe 20 na 21 Julai 2025, akiwa nyumbani kwake, maeneo ya Nyakato, ambapo alimuita mtoto huyo sebuleni kwake na kutekeleza kitendo hicho cha kikatili.
Wakili Changali alieleza kuwa mshtakiwa alitumia fursa ya kutokuwepo kwa bibi na mlezi wa mtoto huyo ambaye mara kwa mara huwa anahudhuria ibada kanisani kwa kumvizia na kumuita mtoto huyo ndani kwake, kisha kumfanyia ukatili huo.
Mshtakiwa katika Kesi hiyo yenye namba 20028/2025 ameshtakiwa kwa shtaka moja la kulawiti, kinyume na kifungu cha 154(1)(a)(2) cha sheria ya kanuni ya adhabu, sura ya 16, marejeo ya mwaka 2023.
Hata hivyo mshtakiwa alikana mashtaka aliyosomewa dhidi yake, ingawa alikiri kumfahamu mtoto husika,upande wa mashtaka uliieleza kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika na kuomba mshtakiwa asomewe hoja za awali.
Katika hoja hizo, ilibainika kuwa mshtakiwa ni jirani wa bibi wa mtoto huyo, Bi Asteria na alikamatwa na Jeshi la Polisi mnamo tarehe 21 Julai 2025, alifikishwa kituo cha polisi Nyakato na Kirumba kisha kuhojiwa kwa tuhuma hizo kabla ya kufikishwa mahakamani.
Baada ya kusomewa hoja hizo, Mh.hakimu alieleza kuwa kesi hiyo ina dhamana, ambapo mshtakiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye kitambulisho cha taifa, barua ya utambulisho kutoka kwa muajiri na kila mmoja kusaini hati ya dhamana ya shilingi milioni tano kwa kuwa mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti hayo, alipelekwa rumande.
Kesi hiyo imepangwa kutajwa tena tarehe 1 Septemba 2025 kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa upande wa mashahidi.