Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo A. Saqware, akizungumza katika kikao kazi kati ya Jukwaa la Wahariri na mamlaka hiyo kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, kilichofanyika leo Agosti 18, 2025 katika ukumbi wa PSSSF Mwenge jijini Dar es Salaam.
Sabato Kosuri Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano Ofisi ya Msajili wa Hazina akifafanua baadhi ya Mambo katika kikao kazi hicho.
………….
Na John Bukuku- Dar es salaam
Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo A. Saqware, akizungumza katika kikao kazi kati ya Jukwaa la Wahariri na mamlaka hiyo kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, kilichofanyika leo Agosti 18, 2025 katika ukumbi wa PSSSF Mwenge jijini Dar es Salaam, amesema kuwa Serikali imeanzisha konsortiamu ya Bima ya Kilimo ili kuhakikisha uendelevu wa miradi pamoja na miundombinu, hatua inayolenga kuhudumia wakulima na kupunguza athari za majanga ya asili.
konsortiamu hiyo ni umoja wa makampuni ya bima yanayotoa bima za kilimo, ambapo jumla ya makampuni kumi na tano yameunda mtaji mkubwa kwa ajili ya kulipa fidia kutokana na majanga yatokanayo na kazi za kilimo. Hatua hiyo inalenga kuongeza tija katika sekta ya kilimo na imekuwa juhudi muhimu sana kwa taifa.
Pia ameeleza kuwa Tayari wakulima wa tumbaku mkoani Tabora wameanza kulipwa fidia kutokana na majanga yaliyosababishwa na mvua kubwa, huku wakulima wa pamba wakinufaika kwa kulipwa baada ya kuathiriwa na wadudu waharibifu. Hii ni miongoni mwa hatua muhimu zilizochukuliwa na Serikali ili kuhudumia wananchi.
Serikali pia imeanzisha konsortiamu ya Mafuta na Gesi, umoja unaojumuisha zaidi ya makampuni ishirini na mbili yaliyotengeneza mtaji wa pamoja kwa lengo la kuhakikisha sekta ya mafuta na gesi inavuna fursa zilizopo nchini.
Aidha amebainisha kuwa Makampuni hayo ya mafuta na Gesi yamewekeza mtaji ili kushiriki biashara ya mafuta na gesi, ambayo awali imezoeleka kufanywa na kampuni za kigeni. Kupitia umoja huu wa makampuni, Shell na washirika wake wanatarajiwa kushiriki kikamilifu katika uchumi wa mafuta na gesi wa Tanzania. Serikali imetajwa kustahili pongezi kwa kuridhia kuanzishwa kwa hatua hiyo.
Mbali na hayo, hatua nyingine muhimu iliyochukuliwa na Serikali ni “kuimarishwa kwa mifumo ya TEHAMA, kufuatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo jumla ya taasisi 30 zinatarajiwa kuunganishwa ili kusomana katika mfumo huo” amesema