WAKAZI wa Sinza E, jijini Dar es Salaam, wameibua maswali mazito wakilalamikia kuvamiwa kwa eneo lililokuwa likitumika kama ofisi za Serikali ya Mtaa, huku wakibaki na wasiwasi kuhusu ofisi zao mpya zilipo na namna huduma zitakavyotolewa.
Akizungumza leo, Agosti 18, 2025, mbele ya waandishi wa habari, Paul Luvinga, mkazi wa eneo hilo, amesema eneo hilo limevamiwa tangu Mei mwaka huu, licha ya kuwa hapo awali ndiko kulikokuwepo ofisi za Serikali ya Mtaa wa Sinza E.
Kwa mujibu wa Luvinga, Mwenyekiti na Mtendaji wa mtaa huo walipokea barua ya kuondoka katika eneo hilo kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo. Hata hivyo, amesema wananchi hawakuwahi kushirikishwa katika uamuzi huo wala kupewa maelezo ya kina kuhusu barua ya awali iliyorejelewa katika nyaraka hiyo.
“Kwenye barua hiyo hakuna kiambatanisho cha kumbukumbu namba iliyorejelewa. Hii inatupa wasiwasi kwamba huenda ni kitu kilichopikwa ndani ya ofisi za mtaa zetu wenyewe,” amesema Luvinga.
Ameongeza kuwa kinachowachanganya zaidi ni taarifa kwamba ofisi ya Mkurugenzi imepokea nyaraka za mahakama zinazoeleza kuwa eneo hilo si mali ya Halmashauri, kinyume na hukumu ya Mahakama Kuu ya mwaka 2003 iliyotamka eneo hilo kuwa ni mali ya serikali ya mtaa.
“Inakuwaje hukumu ya Mahakama Kuu isipuuzwe? Leo tunaambiwa serikali ya mtaa ihame bila kupewa ufafanuzi wa kisheria. Huduma za wananchi sasa zitapatikana wapi?” amehoji.
Mkazi mwingine, Robarth Ngoti, amesema hatua hiyo imeumiza wananchi kwa kuwa serikali ya mtaa ndiyo msingi wa huduma kwa jamii.
“Hili jambo ni fedheha. Serikali za mitaa haziwezi kuhamishwa kwa manufaa ya mtu binafsi bila kushirikisha wananchi. Hata Rais Samia akipata taarifa hizi, ninaamini atashangaa kwa sababu serikali haiwezi kudharauliwa kwa namna hii,” amesema Ngoti.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shina namba 8, Dorah Ndanshau, amesema wananchi wa Sinza E kwa sasa wapo gizani kwani hawajui ofisi mpya zimehamia wapi.
“Hii si sahihi. Barua ya Mkurugenzi haioneshi ofisi zimehamia wapi. Haiwezekani ofisi za serikali ya mtaa kuhamishwa kienyeji kama mpangaji anavyofukuzwa bila taarifa. Wananchi tunataka kujua ofisi zetu ziko wapi,” amesema Dorah.
Michuzi Media ilipotaka ufafanuzi, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Sinza E, Clement Kavishe, alikiri kuhamishwa kwa ofisi hizo lakini hakuweka wazi zimehamia wapi. Wakati huo huo, Mtendaji wa mtaa huo, Amina Juma Mwinyimvua, alipoulizwa alikataa kuzungumza na kuamua kukata simu.
Wananchi wa Sinza E sasa wanaiomba Serikali Kuu na Rais Dkt. Samia kuingilia kati ili kulinda eneo lao na kuhakikisha huduma za serikali ya mtaa zinarejea kama kawaida.