
Kivumbi kimezuka tena kati ya staa namba moja wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz na msanii wake wa zamani wa WCB, Mbosso, baada ya Diamond kumchana waziwazi akidai anatafuta ugomvi wa makusudi ili apate umaarufu wa haraka.
Akizungumza kupitia mahojiano, Diamond alisema baadhi ya maneno na vitendo vya Mbosso havina nia njema bali vimekusudiwa kumhusisha yeye ili kuzua gumzo mitandaoni.
“Unajua kuna watu wanaona wakinitaja au wakijaribu kuleta beef na mimi ndiyo njia pekee ya kupata attention. Lakini hiyo ni trend za kijinga. Mimi siwezi kushindana na mtu kwa mambo yasiyo na maana,” alisema Diamond kwa ukali.
Kauli hiyo imeibua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, huku baadhi ya mashabiki wakiamini bifu hili linaweza kuwa na chanzo cha kibiashara, huku wengine wakihisi ni mkakati wa Mbosso kurudisha jina lake kwenye headline.
Hata hivyo, Diamond alisisitiza kuwa yeye hatopoteza muda wake kwenye malumbano yasiyo na tija, akiongeza kuwa lengo lake kubwa kwa sasa ni kutangaza muziki wake kimataifa na kuendelea kupanua milango ya mafanikio kwa wasanii wa Tanzania.
Kwa upande wake, Mbosso bado hajajibu moja kwa moja kauli ya Diamond, hali inayoacha mashabiki wakiwa na hamu ya kusikia atasemaje au atajibu kwa ngoma mpya kama ilivyo desturi kwenye bifu nyingi za muziki.
Kwa sasa macho na masikio ya mashabiki yapo WCB, wakisubiri kuona iwapo huu utakuwa mwanzo wa vita vipya vya maneno au ni mbwembwe za kiki za kawaida zinazozunguka tasnia ya burudani Bongo.