Benki ya Equity imeandaa kongamano maalum kwa ajili ya wafanyabiashara na wajasiriamali, likiwa na lengo kuu la kuwajengea uwezo wa namna ya kukuza biashara na kupata fursa za kifedha kupitia mikopo.
Kongamano hili limekusanya wadau mbalimbali kutoka sekta ya biashara na fedha kwa ajili ya kujadili changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wengi nchini, hususan tatizo la kutopata mikopo kutokana na kukosa utambulisho wa kifedha.
Meneja Mkuu Biashara wa Benki ya Equity, Leah Ayoub, akizungumza katika kongamano hilo, alieleza wazi kuwa changamoto kubwa inayowakwamisha wafanyabiashara wengi ni kutokutambulika katika mifumo ya benki.
Leah amesema sema wajasiriamali wengi hawajengi historia ya kifedha kwa sababu fedha zao haziendi kupitia benki, jambo linalosababisha wakose rekodi ya kuonyesha mwenendo wa biashara zao na alisisitiza kuwa Equity imejipanga kusaidia kundi hilo kwa kuwapatia elimu ya kifedha na mifumo rahisi ya kibenki ili kuwawezesha kukidhi vigezo vya kupata mikopo.
Kwa upande wake, Bi. Emerald Mutajwaa, Meneja Biashara wa Benki ya Equity Mkoa wa Mwanza, alieleza kuwa benki hiyo imekuwa ikijikita katika kutoa huduma karibu zaidi na wateja ili kuhakikisha wajasiriamali wa mikoani pia wanapata nafasi ya kujipatia mikopo.
Alisisitiza kuwa lengo la benki ni kuhakikisha kila mfanyabiashara, mdogo au mkubwa, anapata nafasi ya kutumia huduma za kibenki ili kuboresha biashara yake.
Akichangia mjadala, Kechu Nkya, mmoja wa wafanyabiashara waliopata nafasi ya kushiriki, alieleza kuwa elimu ya namna ya kujenga historia ya kifedha ni muhimu sana kwa wajasiriamali. Alisema mara nyingi changamoto kubwa siyo ukosefu wa mtaji pekee, bali kutokuelewa taratibu za kibenki.
Kechu aliongeza kuwa kongamano hilo limempa mwanga mpya kuhusu umuhimu wa kutumia benki katika kila hatua ya biashara ili kujiwekea sifa ya kupata mkopo kwa urahisi.