Na Meleka Kulwa, Dodoma
Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imewahakikishia wadau wa sekta ya ununuzi wa umma kuwa moduli mpya ya usimamizi wa mikataba kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Manunuzi ya Umma (NeST) itasaidia kuondoa changamoto za ucheleweshaji wa miradi na upotevu wa mikataba, hatua itakayoongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Akifungua mafunzo ya moduli hiyo jijini Dodoma kwa niaba ya taasisi 30 za serikali zinazoshiriki kwenye mpango huo, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw. Dennis Simba, alisema mfumo huo wa kidijitali unalenga kuongeza uwazi, ufanisi na uwajibikaji katika usimamizi wa mikataba ya umma.
Amesema moduli hiyo itapunguza matumizi ya karatasi na kuweka kumbukumbu za mikataba katika mfumo wa kidijitali, hatua itakayoongeza usalama wa taarifa na urahisi wa upatikanaji wake. Pia itawezesha tathmini ya utendaji wa wakandarasi na kuweka mazingira ya kufungwa kwa mikataba kwa uwazi zaidi.
Bw. Simba alibainisha kuwa changamoto zilizokuwapo, ikiwemo ucheleweshaji wa utekelezaji wa mikataba, mabadiliko ya vifungu bila kufuata taratibu, na malipo yasiyoendana na kazi zilizotekelezwa, zimechangia kupotea kwa rasilimali na kushuka kwa ubora wa huduma kwa wananchi.
“Kwa kutumia NeST, taarifa zote za utekelezaji wa mkataba zitapatikana kwa wakati halisi, hatua kwa hatua,” alisema.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo Bi. Yusta Magehema na Bw. Zefania Paul, walipongeza hatua hiyo wakisema inaleta mageuzi makubwa katika sekta ya ununuzi wa umma, ikiwemo kulinda mazingira, kupunguza mianya ya rushwa na kuhakikisha usawa katika mchakato wa tenda za serikali.