Farida Mangube, Morogoro.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Haki za Binadamu ya Denmark, imeandaa mkutano wa wadau wa haki za binadamu na biashara uliofanyika mjini Morogoro, kwa lengo la kujadili uhakiki wa haki za binadamu katika shughuli za kibiashara.
Mkutano huo umehusisha washiriki kutoka sekta za kilimo, usafirishaji, viwanda, biashara pamoja na taasisi za serikali zinazohusika na usimamizi wa shughuli za kibiashara nchini.
Akifungua kikao hicho, Makamu Mwenyekiti wa THBUB Mhe. Mohamed Khamis Hamad amesema mjadala wa haki za binadamu katika biashara ni hatua muhimu kwa taifa kwani unasaidia kujenga misingi ya uwajibikaji na maendeleo yenye kuzingatia utu wa kila mtu.
“Haki za binadamu ni sehemu ya maisha ya kila mmoja wetu. Kila sekta ina wajibu wa kuhakikisha haki hizo zinalindwa na kuheshimiwa, iwe kwa wafanyabiashara, wafanyakazi, wakulima au wananchi wa kawaida. Tunapozingatia hili, tunaweka msingi imara wa maendeleo ya nchi,” amesema Makamu Mwenyekiti
Kwa upande wake, Katibu wa Tume, Bw. Patience Ntwina, ameeleza kuwa majadiliano hayo yameangazia masuala ya msingi ikiwemo kulinda mazingira, kuzuia ajira za watoto, kuimarisha usalama kazini na kuhakikisha shughuli za kibiashara haziathiri maisha ya wananchi.
“Uchumi hauwezi kukua bila kuheshimu utu wa binadamu. Migogoro kazini, migomo ya wafanyakazi au uharibifu wa mazingira ni dalili ya kukosekana kwa haki. Tunataka kila taasisi na kampuni iwe na uwajibikaji wa kijamii na kiuchumi,” alisema Ntwina
Wadau kutoka sekta binafsi walisisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali na wafanyabiashara ni nguzo kuu ya kufanikisha utekelezaji wa maazimio yanayotokana na mkutano huo.
“Biashara haziwezi kustawi katika mazingira yenye migogoro. Haki za binadamu zinapopewa kipaumbele, wafanyakazi hufanya kazi kwa ufanisi, wawekezaji wanapata uhakika na jamii inanufaika kwa ujumla,” alisema mmoja wa washiriki kutoka sekta binafsi.