*Kaya 1,227 kunufaika na mradi wa Umeme Jua Lindi
*REA kusambaza Majiko Banifu 5,576 Lindi*
*Kila wilaya kugawiwa Majiko Banifu 1,115
Lindi
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imepeleka Mkoani Lindi Mradi wa Umeme Jua wenye thamani ya shilingi milioni 801.74 katika visiwa vyote vitano vilivyopo wilayani Kilwa ikilenga kuongeza upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo ambayo yapo mbali na Gridi ya Taifa na kuhamasisha matumizi ya teknolojia safi kupitia mifumo ya umeme jua.
Akizungumza wakati akipokea taarifa ya mradi huo Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Bi. Zuwena Jiri amekiri kupokea mradi huo na kutoa wito kwa wananchi mkoani humo hasa wakazi wa Visiwani kuchangamkia fursa hiyo kwani tayari Serikali imetoa ruzuku.
“Kila kaya itakuwa na mfumo wake wa kujitegemea, wito wangu kwa wananchi hasa wakazi wa visiwani tuchangamkie fursa iliyokuja, kama mmoja angekuwa anafunga mwenyewe mfumo wa umeme jua inawezekana ikawa gharama kubwa sana lakini Serikali imetoa ruzuku mpaka asilimia sabini na tano (75%)”. Amesema Bi. Zuwena.
Sambamba na hilo Bi.Zuwena amewataka wananchi wa Mkoa wa Lindi kuchangamkia fursa ya Majiko Banifu ambapo serikali imetoa ruzuku ya 85% na kufanya gharama ya Jiko moja kuuzwa kwa Shs 9000 tofauti na bei halisia Shs 60000.
Kwa upande wake, Meneja wa Teknolojia za Nishati kutoka REA, Mha. Michael Kyessi amesema mradi unategemea kusambaza Majiko Banifu 5,576 kwa Mkoa wa Lindi ambapo Majiko 1,115 yatagawanywa kwa kila wilaya.
“Gharama ya mradi kwa mkoa wa Lindi ni shilingi 346,560,000.00 ambapo Serikali itatoa ruzuku ya shilingi 294,576,000.00 . Mtoa huduma ni Tango Energy Ltd ambapo jumla ya majiko banifu 5,776 yatauzwa kwa wananchi kwa bei ya ruzuku. Gharama ya jiko moja ni TZS 60,000 kabla ya ruzuku, hivyo serikali itatoa ruzuku ya asilimia 85 sawa na TZS 51,000 na mwananchi atanunua jiko hilo kwa shilingi 9,000. Majiko haya yatasambazwa katika wilaya tano za Mkoa wa Lindi”. Amesema Mha. Kyessi.
Kuhusu mradi wa jua ambao utafikia kaya 1,227 ndani ya visiwa vitano mkoani humo, Mha. Kyessi amebainisha mifumo hiyo imegawanyika katika mafungu matatu ya uwezo wa nishati ambayo ni 50Wp, 80Wp na 100Wp. Jumla ya mifumo ya 50Wp ni 736, 80Wp ni 307 na 100Wp ni 184.
“Gharama ya ruzuku imetolewa kwa asilimia na kila atakayefungiwa mfumo wa uwezo wa Wati hamsini (50Wp) atapata ruzuku ya 75%, mfumo wa Wati themanini (80Wp) atapata ruzuku ya 65% na mfumo wa Wati mia moja (100Wp) atapata ruzuku ya 55%”. Amesema Mha.Kyessi
Gharama za mradi kwa mkoa wa Lindi ni shilingi miilioni 801.74 ambapo ruzuku ni shilingi milioni 544.21 sawa na asilimia 68 ya gharama zote ya mradi na shilingi milioni 257.53 ni fedha toka kwa wanufaika.
Katika Mkoa wa Lindi mradi huo unategemea kuhudumia visiwa vitano na mtoa huduma mmoja ambaye anategemea kuhudumia visiwa hivyo kupeleka jumla ya mifumo 1,227 ndani ya kipindi cha miaka miwili.