Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari amewakumbusha watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kufanya kazi na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na ushirikiano ili kuleta matokeo chanya zaidi.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa rai hiyo wakati akizungumza katika kikao na Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali kilichofanyika Jijini Dodoma tarehe 18 Agosti, 2025.
*Niwakumbushe watumishi kuendelea kutekeleza majukumu kwa ufanisi na ushirikiano, tuendelee kuzingatia Weledi na Ubora.”* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametumia kikao hicho kuwafahamisha rasmi Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa iliyokuwa Divisheni ya Uandishi wa Sheria imekuwa Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria na imeanza kutekeleza majukumu yake kuanzia tarehe 1 Julai, 2025, ambapo ameeleza kuwa lengo la maboresho hayo ni kuongeza tija katika utoaji wa huduma za Uandishi wa Sheria.
*Msije mkafikiria kuwa Ofisi ya Mwandishi wa Sheria imeondoka moja kwa moja, ni sehemu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kinachofanyika kitaalamu kinaitwa functions separation ili kuongeza tija.”* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Vilevile Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mwandishi wa Sheria zitaendelea kuimarisha mahusiano ili kuhakikisha kwamba ufanisi unaotarajiwa katika Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria unaonekana.
Akifunga kikao hicho, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samwel M. Maneno aliwasisitizia Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuisoma na kuielewa Dira 2050 ili waweze kuitekeleza Dira hiyo kwa ufanisi mkubwa.
*Nawakumbusha watumishi wote kuipitia na kuisoma Dira ya 2050 na kuielewa vizuri na hata kipindi mnatoa Ushauri wa Kisheria kuhusiana na Dira hii mtoe Ushauri utakaokuwa sahihi katika utekelezaji wa Dira.”* Amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katika hatua nyingine, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliwasisitiza watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kushiriki katika mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo yaliyoanishwa katika mpango kazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili waweze kuongeza ujuzi na kuwawezesha kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
*Niwaombe watumishi wa Ofisi hii muendelee kutumia fursa hii ya mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo sisi viongozi wenu tutahakikisha watumishi wote mnapata mafunzo haya ili muweze kutekeleza majukumu yenu kwa ufasaha.”* Amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Awali, Mwandishi Mkuu wa Sheria Bw. Onorius Njole, akitoa wasilisho kuhusiana na uanzishwaji wa Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria amesema kuwa kuanzishwa kwa Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria ni mojawapo ya jitihada za Serikali katika kuendelea kuimairisha na kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Sambamba na hilo, Mwandishi Mkuu wa Sheria amesema kuwa kuanzishwa kwa Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria kutawezesha utekelezaji wa masuala ya Uandishi wa Sheria, Urekebu wa Sheria na Ufasili wa Sheria kwa uwanda mpana zaidi.
*“Kuanzishwa kwa Ofisi hiii kutaongeza na kuwezesha masuala ya uandaaji wa Miswada, Urekebu wa Sheria na Ufasiri wa Sheria kutekelezwa kwa upana wake kwa kuwa tutakuwa na wataalamu wa kutosha.”* Amesema Mwandishi Mkuu wa Sheria