Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Dkt. Joyce Nyoni.
…………..
Na Mwandishi wetu
Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW) ni miongoni mwa vyuo bora ambavyo vinatoa wataalamu mbalimbali wanaoisaidia jamii kutoka katika changamoto kwa kuleta suluhu hasa za kisaikolojia.
Katika kuendelea kuhudumia jamii na kuifanya kuwa bora zaidi, Chuo hicho kimeanzisha program nyingine nne mpya katika mwaka wa masomo wa 2025 /2026.
Program hizo zinalenga katika kuongeza wigo wa wataalamu wa kuhudumia jamii katika nyaja za kutatua migogoro na njia mbadala za kutafuta suluhu ya migogoro,mafunzo ya biashara na ujasiriamali,malezi na makuzi ya awali ya watoto, pamoja na ushauri wa kisaikolojia.
Hatua hiyo ni muhimu sana kwa maendeleo ya jamii kwani wataalamu watakaozalishwa watakuwa na uwezo wa kushughulikia masuala ya malezi ya watoto,utatuzi wa migogoro,saikoloji na namna bora ya kuingiza kipato hasa katika ngazi ya kaya.
NJIA MBADALA ZA KUTATUA MIGOGORO NJE YA MAHAKAMA
Akizungumza na mwandishi wa makala haya, Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo cha Ustawi wa Jamii, Idara ya taaluma za kazi,Asteria Mlambo amesema idara hiyo imeanzisha program mpya inayolenga kutatua migogoro kwa kutumia njia yingine tofauti na mahakama (Conflict Management and Alternative Dispute Resolution).
Bi. Mlambo alisema program hiyo inalenga kuongeza ujuzi na utaalamu wa kutatua migogoro mbalimbali kwa kutumia njia mbadala.
“Utaratibu wa sasa kesi zote zikiwemo za ardhi, kijamii kama vile ndoa
zinatatuliwa na mahakama. Hata hivyo, kutokana na maendeleo na ongezeko la watu na uhitaji, mahakama imeelemewa na kwamba kumekuwepo na milolongo mirefu ambayo inasababisha upotevu wa muda na fedha pia.
Anaongeza “Na mara nyingi wakimaliza kutatua migogoro kwa njia ya kimahakama mahusianano baina ya watu hao yanaharibika kwasababu mara nyingi njia hii inatoa fursa kwa mtu mmoja, mwenye haki, kushinda.
Bi. Mlambo amesema faida kubwa ya kutumia njia mbadala ya kutatua migogoro ni kurudi kwenye mahusiano mazuri kwasababu njia hii inahusisha upatanishi, huokoa gharama na muda unaotumika katika kuendesha shauri.
Jengo la utawala la Chuo cha Ustawi wa Jamii Kampasi ya Dar-es- Salaam.
Anabainisha kuwa njia hiyo inazileta pande zote mbili pamoja kwa usuluhishi kwa kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa. Hata ikitokea mahusiano yao yakaishia pale, wote watabaki kwa namna ambayo bado wataendelea kuwasiliana na kuzungumza bila kikwazo chochote.
“Mfano migogoro ya ndoa mara nyingi tukipelekana mahakamani kuna namna tutaanikana na mtu hatatamani tena kuwa na mawasiliano na mwenzake kutokana na kusema baadhi ya vitu katika sehemu ya wazi,”anasisitiza Mlambo.
Aidha ameendelea kueleza kuwa katika utatuazi kwa njia mbadala inahusisha usiri katika kuzungumza kati ya wenye mgogoro na msuluhishi ambapo ikifika hatua upande mmoja umeshindwa bado utakuwa salama kuendelea kushirikiana na upande ulioshinda.
Anafafanua kuwa program hiyo itatolewa kuanzia ngazi ya Cheti hadi Shahada ambapo wahitimu wataweza kufanya kazi ndani ya jamii.
“Wanaweza kuingia katika sehemu yoyote yenye migogoro mfano kwenye ardhi, kuna ndoa,kazi,na biashara. Wanaweza kuingia sehemu yoyote ambapo wanahitajika.
Mhadhiri huyo anasema hivi karibuni serikali inameanzisha Taasisi ya Usuluhishi inayoitwa Tanzania Institute of arbitration ambayo inatoa vyeti vya kuwatambua hawa watatuzi wa migogoro nje ya mahakama au mbadala.
“Wakati Taasisi hii inaanzishwa kuliwa hakuna mahali ambapo watu hawa walipata mafunzo. Kwa hiyo, inawezekana wanasheria au watu wengine wenye ujuzi kwenye eneo la utatuzi wa migogoro walitumika kwa ajili hiyo.
Anasema program hii inaweza kusomwa na watu walio katika fani mbalimbali akitolea mfano kuwa hata mhandisi anaweza pia kusoma na kwamba ikitokea migogoro katika eneo lake la kazi anaweza kutumika kuitatua.
“Lakini pia kuna Tume ya Haki za Binadamu ambayo inashiriki katika kupokea changamoto za wananchi pale dhuluma au kutokuelewana kunapotokea kwa pande mbili ambapo Tume inafanya chunguzi na kusaidia kwenye utatuzi.
Pichani ni Wanafunzi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii wakiwa wanafanya mitihani ya kumaliza muhula wa masomo
PROGRAM YA MALEZI NA MAKUZI YA WATOTO
Program nyingine mpya ni hii ya Malezi na Makuzi ya Watoto walioko chini ya miaka mitatu (Early Childhood Care and Development)
Program hii imeanzishwa baada ya kuonekana changamoto nyingi za malezi na makuzi ya watoto katika jamii ya watoto ambapo kitaalamu uwezo wa mtoto kuwa bora na kuwa na uwezo mkubwa unaanzia katika ngazi ya awali.
Mlambo anasema program hiyo inamtengenezea mtoto misingi ya namna anavyoweza kukua. Ameongeza kwamba hapo awali hapakuwa na taaluma kama hiyo hapa nchini.
“Hapa kuna nafasi ya kuwapatia ujuzi kuhusu namna ya kuwakuza watoto kimwili,kiakili,kihisia na hata kiroho. Program hii itawasaidia kufahamu maendeleo ya watoto. Kwa mfano, mtaalamu katika eneo hili anaweza kufahamu kwamba katika umri fulani mtoto alitakiwa kujua au kufahamu vitu gani. Hii inasaidia kung’amua changamoto za watoto mapema; zikiwa bado hazijakomaa,”anasisitiza.
Anasema mara nyingi watoto wanapata changamoto lakini inakuwa ngumu kwa wazazi na walezi kutambua.
“Mfano katika maendeleo ya lugha, kwa maana ya kuzungumza, mzazi/mlezi anaweza kufanya tathmini kujua kama mtoto anaweza kuwasiliana sawasawa? Program hii itamuwezesha mzazi/mlezi kujua kwamba mtoto wa umri fulani anapaswa kufanya nini na nini na apaswa kuwasiliana kwa kiwango gani. Kwahiyo, kama mtoto anachagamoto kwenye mawasiliano ni rahisi kumtambua mapema na kuweza kumpatia msaada wa haraka.
Vifaa mbalimbali vya kufundishia vinavyotumika katika darasa mfano la Kozi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto.
Anasema mara nyingi wazazi au walezi wanatambua shida za watoto wao wakiwa wmechelewa hivyo wanabaki na historia kwamba hata mmoja wa wanafamilia alikuwa hivyo au yuko hivyo.
” Wataalamu watakaozalishwa wanaweza kufanya kazi katika maeneo ya watoto wadogo kama shule za awali hata shule za msingi ambapo wanaweza kuwa wasaidizi wa watoto katika mashule na hata katika maeneo ya hospitali, mfano katika kliniki za watoto.
PROGRAM YA MASOKO NA MAENDELEO YA UJASIRIAMALI
Program hii ya Masoko na Maendeleo ya Ujasiriamali (Marketing and Entrepreneurship Development) imejikita katika kufundisha elimu ya biashara hasa kwasababu dunia yote sasa imejikita katika biashara na ujasiriamali. Kwa hiyo taaluma hii ni muhimu sana na haiepukiki.
” Watu wengi wanafanya biashara na ujasiriamali lakini mtu anaweza kujiuliza endapo wanafanya ujasiriamali kama inavyotakiwa? Au watapataje fursa kwenye masoko?
Mlambo anasema kozi hiyo inawafundisha kupata ujuzi wa kuchambua na kujua masoko kwa wajasiriamali,watafundishwa namna ya kutunza fedha,kusimamia biashara, kutafuta masoko na kujiunganisha na wateja na kukuza mitaji.
“Watu wajue kuwa ujasiriamali sio kuhangaika na maisha. Watapata ujuzi wa kuwawezesha kuwa wajasiriamali wenye tija katika maisha yao binafsi lakini pia katika Taifa,”ameongeza na kufafanua.
Amebainisha kuwa program hiyo itatolewa kuanzia ngazi ya Cheti hadi Shahada.
Pichani ni wanafunzi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii wakijifunza kwa vitendo kuhusu afya na usalama mahala pa kazi kiwandani.
USHAURI WA KISAIKOLOJIA
Naye Mhadhiri Msaidizi, Amina Abdallah anasema program ya nne ni ushauri wa kisaikolojia (Counselling Psychology) ambayo itamuandaa mwanafunzi kupata maarifa na stadi za kutatua au kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo jamii inakumbana nazo .
“Changamoto hizo zinaweza kuwa za kijamii, kisaikolojia, kitabia ikiwemo hisia. Mwanafunzi atakapohitimu anaweza kutumia ujuzi au maarifa katika kutoa ushauri kwa jamii kulingana na changamoto za jamii ikiwemo masuala ya maadili,tabia ma kufanya tafiti.
Anaongeza “Mfano masuala ya madawa ya kulevya ,mfadhaiko na mwisho wa siku atakuja na majibu ya tafiti au matatizo aliyoyaona.