Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimsikiliza mkazi wa Shinyanga aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH) kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo wakati wa kambi maalumu ya siku tano ya Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayofanyika mkoani Shinyanga.
Baadhi ya wananchi wa mkoa wa Shinyanga wakisubiri kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo zinatolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH) wakati wa kambi maalumu ya siku tano ya Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayofanyika katika Hospitali hiyo.
Afisa Utafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Zabela Mkojera akichukua taarifa za mkazi wa Shinyanga aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH) kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo wakati wa kambi maalumu ya Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga (SRRH).
Baadhi ya wakazi wa mkoa wa Shinyanga wakisoma vipeperushi vya elimu ya magonjwa ya moyo na taarifa mbalimbali za Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa kambi maalumu ya Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga (SRRH).
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Anna Nkinda akigawa vipeperushi vya elimu ya magonjwa ya moyo kwa wakazi wa mkoa wa Shinyanga waliofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga (SRRH) kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo.
………………
Na Mwandishi Maalumu – Shinyanga
19/8/2025 Watu 213 wakiwemo watu wazima 190 na watoto 23 wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa muda wa siku mbili kwenye kambi maalumu ya matibabu inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga (SRRH).
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya kambi hiyo inayofanyika mkoani Shinyanga.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema kati ya watu waliowaona 34 walikutwa na matatizo ya moyo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa na hivyo kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI.
“Tumetoa rufaa kwa watu wazima 26 na watoto nane ambao tuliwakuta na matatizo ya matundu kwenye moyo, mioyo yao kuchoka na hivyo kushindwa kufanya kazi vizuri, moyo kutanuka, valvu za moyo na mishipa ya damu ya moyo kuziba”, alisema Dkt. Kisenge.
“Magonjwa ya moyo ni magonjwa yanayoweza kuepukika endapo utafuata ushauri wa kitaalamu, ninawaomba wananchi mzingatie kula vyakula bora ikiwemo mboga za majani na matunda, kufanya mazoezi japo kwa kutembea dakika 150 kwa wiki, kuepuka uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe kupindukia”.
“Jengeni tabia ya kupima afya zenu japo mara moja kwa mwaka, lala usingizi wa kutosha kitaalamu inashauriwa kulala masaa saba na zuia msongo wa mawazo kwa kufanya hivi utaepuka kupata magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema jana ni siku ya pili tangu wameanza kambi hiyo ya matibabu aliwasihi wananchi wa mkoa wa Shinganya na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kupima afya za mioyo yao katika siku tatu zilizobaki na kuwaomba kutumia fursa hiyo ya thamani kwani huduma ipo karibu na wao.
Kwa upande wa wananchi waliopata huduma katika kambi hiyo walishukuru kwa huduma hiyo na kusema kuwa imewasaidia kufahamu afya za mioyo yao na kuwapunguzia kufuata huduma hizo jijini Dar es Salaam.
“Ninashukuru kwa huduma niliyoipata ni nzuri, nimefika hapa mapema nimepima vipimo vyote vya moyo na nimeonana na mtaalamu ambaye amenipa elimu ya magonjwa ya moyo na kunianzishia dawa kwani moyo wangu umekutwa na tatizo la kuziba kwa mshipa wa damu nimepewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI”, alisema John Jilanga mkazi wa Kahama.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutuletea wataalamu wa moyo katika mkoa wetu wa Shinyanga, ninaomba huduma hizi ziwe endelevu pia watuletee na wataalamu wa magonjwa mengine yakiwemo ya mifupa”, alishukuru Mary Masanja mkazi wa Kishapu.