Shirika la Reli Tanzania linatarajia kuajiri wafanyakazi 2,460 katika mradi wa reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) kwa vipande viwili vya kutoka Dar es Salaam mpaka Makutopora.
Ajira hizo ni mbali na zaidi ya ajira 115,000 ambazo tayari zinatokana na mkandarasi katika kipande cha kwanza mpaka cha sita.
Katika ajira hizo 2,460 utekekezaji wake ni awamu ambapo katika mwaka wa fedha 2024/25 zaidi ya watumishi 500 wameshaajiriwa na mwaka huu wa fedha 2025/26 matarajio ni kuajiri watumishi 272 na TRC itaendelea kuajiri mpaka kufikia watumishi 2,460.
Wakati utekekezaji wa utoaji ajira rasmi za Shirika ukiendelea, jumla ya ajira 115,000 kutoka mkandarasi zimeshawanufaisha Watanzania 115,000 zikiwemo za vijana wa elimu ya darasa la saba na viwango vingine vya elimu katika fani mbalimbali.
Mchanganuo wa ajira hizo 115,000 kutoka kwa mkandarasi ni kwamba ajira 35,000 ni za moja kwa moja na zaidi ya 80,000 ni zisizo za moja kwa moja zikijumuisha makundi mbalimbali kama baba na mama lishe, bodaboda, bajaji na watoa huduma za makampuni mbalimbali ya mawasiliano kama mocha, line za simu n.k.
Utoaji wa ajira hizo ni utekelezaji wa maagizo na maelekezo ya serikali kwamba miradi yote ambayo serikali imewekeza iwe na manufaa kwa Watanzania hususani wale wanaoishi kuzunguka miradi husika na wengine kutokana na ujuzi unaohitajika kwa viwango vya elimu na ujuzi wao.