WAZIRI wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Prof.Adolf Mkenda akizungumza kwenye jukwaa hilo jijini Arusha.
Mkurugezi wa Taasisi ya WAJIBU, Ludovick Utouh akizungumza kwenye jukwaa hilo.
…….
Happy Lazaro, Arusha .
WAZIRI wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Prof.Adolf Mkenda,amesema kuwa ,tusipojenga utamaduni wa kuchukia rushwa na ufisadi tutazipeleka nchi zetu pabaya,hivyo tunapaswa kuwa wamoja katika kuzilinda mali za Umma na tuepuke kuzitafuna wenyewe na kuzitumia kwa manufaa yetu binafsi.
Prof.Mkenda ameyasema hayo jijini Arusha wakati akizungumza kwenye Jukwaa la mkutano wa Taasisi ya WAJIBU uliowakutanisha wanafunzi kutoka vyuo 11 vya Elimu ya Juu hapa nchini.
Amesema kuwa,matumizi mabaya ya rasilimali za Umma imekuwa chanzo kikuu cha kuzidi kudidimiza na kurudisha nyuma maendeleo kwa nchi za Bara la Afrika.
” kama nchi inataka kuibua viongozi ambao ni wa kweli na watakaolinda rasilimali na kuongoza vizuri ni lazima kujenga tabia nzuri kwa watu wote wakiwamo vijana kwa kuwa kundi la vijana wako takribani asilimia 40.”amesema Prof .Mkenda .
“Tusipojenga utamaduni huu wa kuchukia rushwa na ufisadi tutazipeleka nchi zetu pabaya,hivyo basi tunapaswa kwa pamoja na umoja wetu kuzilinda mali za Umma na tuepuke kuzitafuna wenyewe na kuzitumia kwa manufaa yako binafsi,”ameongeza.
Aidha amefafanua wakati mwingine kasoro zinatokea kwa kutokuwepo kwa mifumo mizuri ya kiutendaji kazi na kiutawala.
“Wakati mwingine fedha zinapotea kwa kutokuwepo kwa mifumo mizuri na sio wizi ila ni kwa sababu mfumo sio mzuri hasa mifumo ya utoaji fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo,”amesema.
Naye Mkurugezi wa Taasisi ya WAJIBU,Ludovick Utouh,amesema Jukwaa hilo lilianzishwa mwaka 2021 likiwa na lengo la kuandaa vijana kuwa viongozi bora wenye uadilifu,uwajibikaji na uzalendo kupitia mafunzo wanayopata kupitia vilabu vyao vya uwajibikaji.
Ameongeza kuwa, kupitia Jukwaa hilo,wanawajengea vijana uwezo kuhusu dhana ya uwajibikaji,uadilifu,uzalendo na mapambano dhidi ya rushwa,pia ushiriki wa vijana katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo ikiwamo michakato ya upangaji wa bajeti kitaifa hadi ngazi ya vijiji na kushirikia katika michakato ya kutunga sera zinazohusu maendeleo ya nchi.