Na Pamela Mollel, Arusha
Tamasha la Tanzania Samia Connect 2025 linalotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 21–23, 2025 katika Viwanja vya Mgambo, Uzunguni Jijini Arusha, linatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya wasanii 50 kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Arusha. Miongoni mwao ni wakongwe wa muziki wa Arusha akiwemo Fido Vato anayetikisa na wimbo Chuga Hiyo pamoja na JCB aliyevuma kupitia wimbo Ukisikia Paah.
Kwa niaba ya wakongwe wengine wa muziki mkoani Arusha, wasanii hao wameahidi kutoa burudani ya kipekee kwa kila mshiriki atakayefika kwenye tamasha hilo. Wamewataka pia vijana wenye vipaji kujitokeza kwa wingi kuonesha uwezo wao, wakieleza kuwa Tanzania Samia Connect ni jukwaa muhimu la kukuza na kuibua vipaji vipya.
Aidha, Fido Vato na JCB wamempongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Kenani Laban Kihongosi, kwa ubunifu na uongozi wake katika kuratibu tamasha hilo. Wamesema Tanzania Samia Connect ni mkombozi kwa wananchi kwani mbali na burudani, litahusisha pia utoaji wa huduma mbalimbali za serikali ikiwemo matibabu, hati na nyaraka muhimu kama vile Vitambulisho vya Taifa.
Wakongwe hao wa muziki wameeleza kuwa tamasha hilo si tu linainua sanaa na muziki wa Arusha, bali pia ni kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi kutokana na ugeni mkubwa utakaovutia wageni kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi.