Na WAF, – Songwe
Serikali kupitia Baraza la Optometria nchini imefurahishwa na huduma za Optometria zinazotolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe baada ya Hospitali hiyo kuwa kielelezo thabiti cha huduma bora za Optometria na mfano wa kuigwa nchini.
Pongezi hizo zimetolewa Agosti 20, 2025 baada ya Msajili wa Baraza la Optometria Bw. Sebastiano Millanzi na jopo lake , kufanya zoezi la usimamizi shirikishi katika hospitali hiyo na kujionea huduma zenye kuzingatia viwango na miongozo ya baraza hilo.
“Tumetembelea sehemu ya huduma za optometria, hatuna budi kusema huduma zinazotolewa zinatia moyo hasa upatikanaji wa miwani tiba ikiwemo wataalam wenye weledi, hili mlipokee na mliendeleze ili wananchi wanapokuja kupata huduma zenu wawe ndio mabalozi wenu,” amesema Bw. Millanzi.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Ramadhan Juma Ramadhani, amefurahishwa na ujio wa Baraza la Optometria katika hospitali yake huku akiahidi kuyaendeleza mazuri yote na kuboresha mapungufu yaliyobainika.
“Mnapo kuja ninyi mnakuwa jicho la pembeni kutufanyia tathmini, pengine sisi tunaweza kujiona tupo sahihi kutokana na mazoea, lakini tukiambiwa na wengine inakuwa sehemu ya kujipima upya” alisema Dkt. Ramadhan.
Mbali ya pongezi hizo jopo hilo pia lilibaini uwepo wa shughuli za utengenezaji miwani unaofanywa kwa njia za siri na watu wasio na utaalamu, uuzaji wa bidhaa za optometria zikiwemo Fremu za Miwani na Lenzi uliokuwa ukitendeka kwa njia ya kificho kwenye baadhi ya vituo mkoani humo.
Aidha wataalam hao pia wamewataka wamiliki binafsi wenye mapungufu ya kitaaluma kujisalimisha katika Ofisi za Waganga Wakuu wa Halmashauri ili kupata maelekezo ya kina ya namna bora ya kutoa huduma za optometria mkoani humo.
Kufuatia hali hiyo Kikosi kazi hicho kimetoa siku tisini (90) kwa kituo cha kutolea huduma za Optometria cha Dova ambacho usajili wake ulibainika kuwa na taarifa zinazokinzana na eneo kituo kilipo.
“Tumebaini baadhi ya mapungufu ambayo yametulazimu kuchukua muda mwingi kutoa elimu kwa mtu anayekiuka taratibu ili aweke mambo yake vizuri na atoe huduma kwa wananchi kulingana na Sheria,” amesema Bw. Millanzi.
Zoezi la Usimamizi Shirikishi mbali ya kukagua na kutoa maelekezo, limetumika pia kuwajengea uwezo watumishi wa Afya ngazi ya mkoa na halmashauri ili waweze kusimamia kikamilifu shughuli za Optometria katika maeneo yao.