Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Benedict Wakulyamba, wakati akizungumza na viongozi wa kimila.
Katibu Tawala mkoa wa Rukwa Msalika Makungu akizungumza wakati wa zoezi la ugawaji wa mizinga ya nyuki
……………..
Na Neema Mtuka Sumbawanga
Rukwa :Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba, ameongoza hafla ya kugawa mizinga 200 ya kisasa ya nyuki kwa viongozi wa kimila (machifu) wa mkoa wa Rukwa ikiwa ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kukuza sekta ya ufugaji nyuki na kuendeleza uhifadhi wa mazingira.
Akizungumza leo Agosti 21,2025 kwenye tukio hilo, CP Wakulyamba amesema hatua hiyo inalenga kuongeza thamani ya sekta ya ufugaji nyuki, kuongeza upatikanaji wa mazao ya nyuki.
Wakulyamba amesema wameamua kuwatumia viongozi wa kimila kama nguzo muhimu katika kulinda na kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Amesisitiza kuwa viongozi hao watasaidia katika kuhakikisha wanalinda vyanzo vya maji,misitu, na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uhifadhi ili kizazi kijacho kirithishwe na rasilimali zilizopo hapa nchini.
“Viongozi hawa watatusaidia kulinda na kuhifadhi kwa kuwa wao ni kioo cha jamii na wana uwezo wa kuwakutanisha wananchi kwa pamoja ili kuelimishana kwa pamoja “.
Afisa Uhifadhi kutoka TFS mkoa wa Rukwa Hussein Msuya ameeleza kuwa zoezi hilo ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kugawa mizinga ya kisasa kwa wadau mbalimbali likiwa na lengo la kuongeza kipato cha wananchi na taifa kwa ujumla.
Msuya amesema kupitia sekta ya ufugaji wa nyuki wanaamini kuwa vijana watapata ajira na kujiingizia kipato huku akisisitiza umuhimu wa utunzaji wa mizinga hiyo na mazingira.
Katibu tawala wa mkoa wa Rukwa Msalika Makungu amewahimiza wananchi kutunza na kuhifadhi mazingira na kuacha tabia ya kufanya shughuli za kibinaadamu kwenye vyanzo vya maji na kila mmoja anapaswa kuwa mlinzi wa mwenzake.
Aidha amewataka viongozi wa kimila kuendelea kuikuza amani iliyopo na kuchochea utulivu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu 2025.
Kwa upande wao, baadhi ya machifu waliopokea mizinga hiyo akiwemo mwene kapufi wa Sumbawanga asilia ameishukuru serikali na TFS kwa kuwathamini na kuwaweka mstari wa mbele katika juhudi za kulinda rasilimali za asili.
Pia ameahidi kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za ufugaji nyuki na uhifadhi wa misitu.