
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mfumo wa kwanza wa usambazaji wa gesi ya LPG kwa wingi katika Soko la Samaki la Kimataita Ferry jijini Dar es Salaam. Uzinduzi huo umefanyika leo Agosti 21, 2025 katika soko hilo Jijini Dar es Salaam, wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo, aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge na Mgombea wa Mbunge wa Jimbo la Ilala kupitia CCM Mussa Zungu na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Elihuruma Mabelya.

Mhandisi wa Mifumo Mikubwa ya Gesi (Bulk Consumer Engineer) Simplis Tesha akitoa Maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila kuhusu tanki la gesi ambalo limefungwa katika Soko la Kimataifa la Samaki Feri jijini Dar es Salaam ambapo wafanyabiashara wa soko hilo watakuwa wananunua gesi kwa kadri wanavyotumia
……..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Kampuni ya ORYX Energies Tanzania, kwa kushirikiana na Serikali na wadau wa soko, imetangaza rasmi uzinduzi wa mfumo wa kwanza wa usambazaji wa gesi ya LPG kwa wingi katika Soko la Kimataifa la Samaki la Ferry, jijini Dar es Salaam.
Mradi huo wa kihistoria ni hatua kubwa katika kuimarisha upatikanaji wa nishati safi kwa wauzaji wa samaki na wajasiriamali wadogo katika soko hilo. Kupitia mfumo huu mpya wa “Lipa Kadri Unavyotumia” (PAYG), wauzaji sasa wanaweza kulipia gesi kulingana na matumizi yao halisi, hatua inayosaidia kuondoa gharama kubwa za kujaza mitungi na kupunguza matumizi ya kila siku hadi Shilingi 45,000.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mfumo huo, ambapo tanki kubwa la gesi limejengwa kwa ajili ya kusambaza gesi kwenye majiko ya wafanyabiashara, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema mfumo huu utawezesha wafanyabiashara kulipa kulingana na matumizi yao binafsi.
“Kila mfanyabiashara sasa ana mita yake inayosoma matumizi ya kila siku, kabla na baada ya matumizi. Hakuna tena kubahatisha au kulazimika kununua mitungi midogo kwa gharama kubwa,” alisema Chalamila.
Aidha, alisisitiza kuwa usalama umepewa kipaumbele, ambapo kila jiko limefungwa valve maalum ya usalama itakayozuia gesi iwapo dharura itatokea. Alisema matumizi makubwa ya gesi yanahitaji tahadhari kubwa, na ORYX imehakikisha vifaa vya kuzima moto na taratibu za dharura vipo tayari.
Chalamila alibainisha kuwa kupitia mfumo huu, ufuatiliaji wa matumizi ya gesi utakuwa rahisi, na gesi itaweza kuletwa kwa wakati ili kujaza tanki kubwa. Wafanyabiashara waliokuwa wakitumia hadi Shilingi 180,000 kwa siku sasa wanaweza kuokoa hadi Shilingi 45,000 kila siku.
> “Kupitia mfumo huu wa Lipa Kadri Unavyotumia, hakuna upotevu tena, hakuna gesi isiyotumika kama ilivyokuwa zamani ambapo gesi ilibaki kwenye mitungi midogo. Usalama uko juu, na sina shaka na utaalamu wa ORYX katika kuhakikisha kila hatua ya usalama imezingatiwa,” aliongeza Mkuu huyo wa Mkoa.
Mkurugenzi Mtendaji wa ORYX Gas, Benoit Araman, alisema lengo la mfumo huu ni kupunguza gharama, kuondoa upotevu na kuongeza ufanisi na usalama wa matumizi ya gesi.
“Mfumo huu wa kisasa umetengenezwa na timu ya mafundi wa ORYX kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa. Umerahisisha uendeshaji, ugavi endelevu na unasaidia pia katika ufuatiliaji wa matumizi pamoja na matengenezo ya haraka,” alisema Araman.
Awali, Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga, kutoka Wizara ya Nishati alieleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi, huku akiipongeza ORYX kwa mchango wake mkubwa katika kuhamasisha matumizi ya gesi safi ya kupikia.
“Tangu kuzinduliwa kwa mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia mwezi Januari 2024, kumekuwa na mafanikio makubwa. Lengo la Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia,” alisema Mhandisi Luoga.
Katika hatua nyingine, aliyekuwa Naibu Spika Mussa Zungu, alisema kuwa awali wafanyabiashara wa soko hilo walifikisha mahitaji yao, na aliamua kuwatafuta ORYX Gas ili kusaidia kutatua changamoto hiyo.