(Geita, Tanzania – Agosti 20, 2025)
Bohari ya Dawa (MSD) leo imemkabidhi rasmi eneo la mradi kwa kampuni ya China ya Hainan International, kwa ajili ya kuanza rasmi ujenzi wa ghala jipya la kisasa lenye ukubwa wa mita za mraba 4,800, litakalohudumia wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Mradi huo wa ujenzi wa ghala jipya ni sehemu mipango ya MSD ys kuongeza miundombinu ya uhifadhi wa bidhaa za afya katika maeneo mbalimbali mchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Bw. Mavere Tukai, amesisitiza umuhimu wa mkandarasi huyo kukamilisha mradi huo kwa wakati, kuzingatia masharti ya mkataba na kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana (value for money) na kuzingatiwa.
“Mradi huu utapunguza kwa kiasi kikubwa mzigo kwenye Kanda ya Mwanza, ambalo kwa sasa inahudumia eneo kubwa la kijiografia,” alisema Tukai.
Tukai ameongeza kuwa ujenzi wa ghala la Chato, utawanufaisha wananchi wa Kanda ya Ziwa kwa huduma za haraka na bora zaidi za ugavi wa dawa, vitendanishi, na vifaa tiba.
Kwa upande wake Chuo Kikuu cha Ardhi (Ardhi University of Dar es Salaam) ambao ndio wasimamizi wakuu wa mradi huo kwa niaba ya MSD, wamebainisha kwamba mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, ukiwa na miezi miwili ya awali kwa maandalizi ya ujenzi (resource mobilization), huku kikihaidi kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ubora wa hali ya juu kama ilivyopangwa.
“Huu ni mradi wetu wa tatu kusimamia kwa niaba ya MSD, na tunashukuru kwa imani yao ya kuendelea kutupa dhamana hii, na tutahakikisha kila hatua ya ujenzi inazingatia viwango vya kitaalamu vilivyowekwa.” Alisema Dkt. Nkini mwakilishi wa Chuo Kikuu cha Ardhi.
Kwa upande wao, kampuni ya Hainan International wameeleza kuwa wana uzoefu mkubwa katika miradi mikubwa ya ujenzi, na wameahidi kufanya kazi kwa bidii usiku na mchana ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
“Tuna rasilimali za kutosha na timu yenye uzoefu wa kutekeleza mradi huu kwa ufanisi mkubwa, hivyi wataendelea kushirikiana kwa karibu na MSD pamoja na wasimamizi kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi ili kuhakikisha malengo yote ya mradi yanatimia.” Alisema msemaji wa Hainan International. “
Mradi huu ni sehemu ya mpango wa Mlalati wa MSD wa kuimarisha huduma za afya kwa kuboresha miundombinu ya kuhifadhi dawa katika maeneo mbalimbali ya nchi, hususan katika Kanda ya Ziwa.