Dar es Salaam, Tarehe 21 Agosti 2025:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inapenda kutoa ufafanuzi wa taarifa potofu kuhusu hali ya baridi inayoendelea nchini. Taarifa hiyo imesambaa kwenye mitandao ya kijamii ikieleza, “kuanzia kesho hadi Agosti 22 mwaka huu 2025 kutakuwa na baridi zaidi kuliko miaka ya nyuma”. Taarifa hiyo potofu imehusisha Aphelion, tukio la Aphelion ni hali ya kawaida katika mzunguko wa dunia kwenye mfumo wa jua (solar system). Hata hivyo, mchango wake katika mwenendo wa hali ya baridi kati ya msimu mmoja na mwingine sio mkubwa katika maeneo yetu.
Kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti kila mwaka, ni majira ya Kipupwe katika maeneo mengi hapa nchini ambapo mifumo ya hali ya hewa hutawaliwa na hali ya baridi na upepo mkali. Utabiri wa msimu wa Kipupwe uliotolewa na TMA tarehe 22 Mei 2025 unaonesha kuwa hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi.
TMA inapenda kuwakumbusha wananchi na wadau wote kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Hali ya Hewa Na. 2 ya Mwaka 2019, TMA ndio taasisi pekee yenye jukumu la kutoa taarifa za utabiri na tahadhari za hali ya hewa kwa Umma na kuwa ni kosa kisheria kusambaza taarifa kutoka katika vyanzo visivyo rasmi kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 27 na 31(5) cha Sheria hiyo.
Imetolewa na:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.