
Mhandisi Mkuu wa Kampuni ya ETDCO, Mustapha Himba (wa pili kutoka kushoto) akitoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa miradi kwa Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, wakati alipotembelea banda la kampuni hiyo katika Maadhimisho ya Siku ya Sekta ya Ujenzi na Maonesho ya Samia 2025 (Samia Construction Sector Day 2025), yaliyofanyika leo, 21 Agosti 2025, katika Ukumbi wa Super Dome, Masaki – Dar es Salaam.


Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa Kampuni ya ETDCO, Mhandisi Dismas Masawe (katikati) akitoa elimu kuhusu utekelezaji wa miradi kwa wadau waliotembelea banda la kampuni hiyo katika Maadhimisho ya Siku ya Sekta ya Ujenzi na Maonesho ya Samia 2025 (Samia Construction Sector Day 2025).

Afisa Uhusiano wa Kampuni ya ETDCO Bi. Samia Chande (kulia) akitoa elimu ya utekelezaji wa miradi kwa wadau waliotembelea banda la kampuni hiyo katika Maadhimisho ya Siku ya Sekta ya Ujenzi na Maonesho ya Samia 2025 (Samia Construction Sector Day 2025).





…………
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, ameipongeza Kampuni ya ETDCO kwa umahiri na weledi katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi, ukarabati na usambazaji wa miundombinu ya umeme nchini.
Aidha, amewasihi viongozi wa Kampuni hiyo kutangaza mchango wao kwa jamii na kutambua kazi kubwa wanayoifanya katika kuimarisha Sekta ya nishati ya umeme.
Mhe. Ulega ameyasema hayo leo, Agosti 21, 2025, jijini Dar es Salaam, alipotembelea banda la Kampuni ya ETDCO katika Maadhimisho ya Siku ya Sekta ya Ujenzi na Maonesho ya Samia 2025 (Samia Construction Sector Day 2025), yanayofanyika katika Ukumbi wa Super Dome, Masaki.
Amesisitiza kuwa ETDCO inapaswa kuendeleza juhudi zake kwa bidii ili kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa Kampuni ya ETDCO, Mhandisi Dismas Masawe, amesema kuwa lengo la kampuni kushiriki maonesho hayo ni kuonesha mchango wa sekta ya ujenzi, pamoja na namna wanavyotekeleza miradi ya miundombinu ya umeme.
Mhandisi Masawe ameeleza kuwa sekta ya ujenzi haiwezi kusonga mbele bila upatikanaji wa umeme wa uhakika, huku akifafanua kuwa ETDCO imefanikiwa kusambaza huduma ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini.
Ameongeza kuwa, katika Awamu ya Sita ya Serikali, kampuni hiyo imefanikiwa kujenga miundombinu ya umeme yenye msongo wa kilovolti 132 kwa jumla ya kilomita 495, kwa kuunganisha huduma ya umeme kutoka Tabora hadi Katavi (km 383), kutoka Tabora hadi Urambo (km 115), pamoja na kupeleka umeme kwenye vitongoji 105 na vijiji 291, hatua iliyochangia kwa kiasi kufikisha huduma hiyo kwenye maeneo ya viwanda nchini.
“Upatikanaji wa huduma ya umeme wa uhakika umechangia kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi, sambamba na kukuza uchumi wa wananchi katika maeneo mbalimbali,” amesema Mhandisi Masawe.